Dalili mrithi wa Gachagua atatajwa Ijumaa
HUENDA nchi ikaadhimisha Mashujaa Dei mnamo Oktoba 20, 2024 ikiwa na naibu wa rais mteule iwapo Seneti itaidhinisha kuondolewa kwa Bw Rigathi Gachagua na Bunge la Kitaifa.
Ingawa Bunge la Kitaifa huwa haliandai vikao Ijumaa, kikao kimeratibiwa wiki hii huku matarajio yakiwa mengi kwamba Rais William Ruto atawasilisha kwa Bunge hilo jina la mrithi wa Bw Gachagua.
Kikao cha Ijumaa kinajiri, siku moja tu baada ya Seneti kufanya uamuzi wake kuhusu mashtaka ya kumuondoa mamlakani Bw Gachagua.
Mnamo Jumanne wiki hii, Kamati ya Shughuli za Bunge (HBC) ilikutana na kubadilisha kalenda yake iwe na kikao Ijumaa wiki hii wakati ambao wabunge wanatakiwa kuwa katika mapumziko mafupi.
Mabadiliko ya kalenda ya Bunge yaliidhinishwa baadaye na Bunge kwenye kikao.
“Kwamba Bunge hili liazimie kufanya vikao Ijumaa Oktoba 18, 2024, kuanzia saa 9.30 asubuhi kwa kikao cha asubuhi na saa nane na nusu jioni kwa kikao cha alasiri, kwa madhumuni ya kuzingatia shughuli za kipaumbele, pamoja na Miswada iliyokubaliwa,” hoja iliyoidhinishwa ya kubadilisha kalenda ya Bunge inasema.
Hii inamaanisha kuwa Bunge sasa litapumzika kwa muda mfupi Jumanne Oktoba 22, 2024.
HBC, inayoongozwa na Spika wa Bunge, hukutana kila Jumanne alasiri wakati Bunge liko kwenye vikao ili kupanga shughuli zitakazofanywa Bungeni.
Ingawa haijabainika ni msimamo gani ambao Seneti itachukua kuhusu mashtaka ya kumuondoa madarakani Bw Gachagua, duru ndani ya bunge zinasema kuwa Bunge hilo litaketi Ijumaa ili kupokea rasmi jina la mteule wa wadhifa wa Naibu Rais kutoka kwa Rais William Ruto.
“Ni ukweli kwamba Wabunge watajulishwa rasmi kuhusu mteule wa unaibu rais siku ya Ijumaa ili kuanzisha mchakato wa kumuidhinisha. Ndio sababu Bunge litakuwa na kikaol Ijumaa, vinginevyo, kwa nini ikae siku kama hiyo?” Mbunge mmoja mwanachama wa HBC alisema.
Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka pia amekashifu kikao cha Ijumaa.
Wamepanga kikao siku ya Ijumaa ili kupokea jina la mteule wa naibu rais hata kabla ya Seneti kutoa msimamo wake kuhusu mashtaka ya kumuondoa naibu rais,” alisema Bw Musyoka.
Kifungu cha 149 cha katiba kinasema ndani ya siku 14 baada ya nafasi ya Naibu Rais kutokea, Rais atamteua mtu wa kujaza nafasi hiyo.
Kisha Bunge litapiga kura kuhusu uteuzi ndani ya siku 60 baada ya kumpokea jina la mteule kutoka kwa rais.
Hata hivyo, hakuna ufafanuzi kuhusu nini kinafanyika ndani ya siku 60 ambazo Bunge linatakiwa kumuidhinisha au kumkataa anayeteuliwa.
Kifungu cha 3 cha Sheria ya Uteuzi wa Umma (Idhini ya Bunge) ya mwaka 2011 kinasema kwamba uteuzi chini ya katiba au sheria nyingine yoyote “ambapo kibali cha Bunge kinahitajika hautafanywa isipokuwa uteuzi huo umeidhinishwa au kuonekana kuwa umeidhinishwa na bunge kwa mujibu wa Sheria hii.”
Ingawa sheria inatoa muda wa siku 14 ambapo wabunge wanatakiwa kuidhinisha uteuzi wa watu wanaohitaji idhini ya bunge, katiba inasema jina la mteule wa naibu rais lazima lizingatiwe ndani ya siku 60.