Makala

Gavana Mutai afunguka kuhusu madai ya kunyanyasa kimapenzi binti wa Kericho

Na VITALIS KIMUTAI, BENSON MATHEKA October 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

GAVANA wa Kericho Erick Mutai ametaja madai ya kushiriki ngono visivyo kuwa ya uongo kutoka kwa wapinzani wake akidai yana nia ya kumchafulia jina, kudhuru familia yake changa na kumharibia maisha yake ya kitaaluma.

Gavana huyo, katika kutaka kusafisha jina lake, Jumatano alisema anatafakari kuwachukulia hatua za kisheria wanasiasa waliotoa madai hayo ambayo hayakuweza kuthibitishwa.

“Ningependa kuishukuru familia yangu, hasa mke wangu, kwa kusimama nami katika wakati huu mgumu sana. Madai yaliyotolewa dhidi yangu yalinisumbua sana,” Dkt Mutai alisema.

Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu aokolewe na Seneti, gavana huyo alidai kuwa wapinzani wake walijiaibisha katika azma yao ya kumwangusha.

“Haikuwa safari rahisi. Nisingefika nilipo na kushinda changamoto bila maombi kutoka kwa familia yangu, marafiki na wafuasi wangu. Mungu ametuwezesha,” Dkt Mutai alisema.

Dkt Mutai alitimuliwa na madiwani 31 kati ya 47 wa Bunge la Kaunti ya Kericho mnamo Oktoba 2, 2024 kufuatia hoja iliyowasilishwa na MCA wa wadi ya Sigowet Kiprotich Rogony, huku madiwani 16 waliomuunga mkono gavana huyo wakisusia kikao hicho.

Dk Mutai alikabiliwa na mashtaka ya ukiukaji mkubwa wa Katiba ya 2010 na sheria nyinginezo, matumizi mabaya ya ofisi, kukiuka Sheria ya Uongozi na Uadilifu, ukiukaji wa Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma, 2012, ubadhirifu wa fedha za umma, kutumia mapato ya kaunti kinyume cha sheria na kujihusisha na vitendo vichafu vya ngono.

Gavana huyo anayehudumu muhula wa kwanza kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) alishtakiwa kwa kumlazimisha mwanamke kufanya ngono bila kinga.

Mwathiriwa ambaye alidaiwa kutoa ushahidi kwa bunge la kaunti alikuwa katika Seneti wakati wa kusikilizwa kwa mashtaka ambapo alitambuliwa tu katika orodha ya mashahidi kama ‘binti wa Kericho’.

Akiwa amevalia buibui na miwani ili kuficha asitambuliwe, shahidi huyo alizua gumzo kwenye mitandao ya kijamii alipofikishwa Bungeni, kwa kile kilichodaiwa kuwa tayari kutoa ushahidi katika kesi inayomkabili gavana huyo.

“Mashtaka yote yaliyotolewa dhidi yangu yalikuwa ya uongo, mbali sana na ukweli. Nilikana mashtaka yote na nilitakaswa na Seneti

“Lakini kutakaswa kwangu hakumaanishi kuwa mimi ni kiongozi kamili. Nina udhaifu na kushindwa kwangu ni kama kiongozi mwingine yeyote na binadamu.

“Kuna masuala katika mashtaka hayo yenye uwezekano wa kuharibu familia. Ninataka kumshukuru mke wangu kwa kuwa mvumilivu na mwenye maombi katika kipindi chote cha propaganda zilizokuwa zikisambazwa.

“Madai ya ngono yalikuwa ya kinyama na ninashauriana na mawakili wangu kwa nia ya kuchukua hatua (za kisheria) dhidi ya walioyatoa,” alisema