Maswali mashahidi wa Bunge Sakaja na Wanjau wakikosa kufika kutoa ushahidi dhidi ya Gachagua
MASWALI mengi yaliibuliwa jana Alhamisi baada ya Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja na Katibu wa Baraza la Mawazi Mercy Wanjau kukosa kufika katika Seneti kutoa ushahidi katika kesi ya kumtimua afisini Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Wawili hao walikuwa wameorodheshwa kama mashahidi wa Bunge la Kitaifa na waliratibiwa kufika katika seneti kuhojiwa na mawakili wa Bw Gachagua kuhusu madai yaliyomo kwenye hatikiapo zao zilizowasilishwa kwa bunge hilo.
Kabla ya kuanza kwa kikao cha alasiri jana, kiongozi wa jopo la mawakili wa Bw Gachagua, Paul Muite alitaka kujua iwapo Bw Sakaja atawasilishwa kutetea ushahidi alitoa kwamba naibu huyo wa rais aliingilia utendakazi wa serikali ya Kaunti ya Nairobi.
“Mheshimiwa Spika, je, Gavana Johnson Sakaja ataitwa ili mawakili wetu kumhoji kuthibitisha madai kwenye hatikiapo yake? Nauliza hivyo, kwa sababu yaliyomo kwenye hatikiapo hiyo yanamharibia sifa Naibu Rais. Ikiwa shahidi huyo hataitwa, tunaomba ushahidi wake uondolewe kutoka kwa rekodi za bunge hili,” Bw Muite akasema.
Duru zilisema Bw Sakaja yuko jijini Mexico City, nchini Mexico, ambako anahudhuria mkutano kuhusu usimamizi wa miji.
Mkutano huo kwa jina, “Bloomberg CityLab 2024 summit” pia unajadili mchango wa vijana katika ustawishwaji wa miji mikuu ulimwenguni.
Katika hatikiapo iliyowasilishwa kwa Seneti, Bw Sakaja anadai Bw Gachagua aliingilia utendakazi wa serikali yake alipopinga uamuzi wa kuhamishwa kwa wafanyabiashara kutoka soko la Wakulima hadi soko jipya lililoko katika barabara ya Kangundo, eneo bunge la Embakasi Mashariki.
Naye Bi Wanjau alimsuta Bw Gachagua kwa kukaidi uamuzi uliofikiwa katika Baraza la Mawaziri wa kuondolewa kwa watu waliojenga makazi ndani ya mita 30 kutoka ukingo wa Mto Nairobi.