Makala

Sherehe na hasira Kindiki akiteuliwa kumrithi Gachagua

Na WAANDISHI WETU October 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAKAZI wa Kirinyaga Ijumaa walimkashifu Rais William Ruto wakimlaumu kwa kumsaliti Naibu wake Rigathi Gachagua.

Walisisitiza kuwa Dkt Ruto ndiye anayepaswa kulaumiwa kwa kutimuliwa kwa Bw Gachagua na kuapa kutompigia kura katika uchaguzi wa 2027.

Walisema inasikitisha kwamba, Dkt Ruto alikataa kabisa kusimama na Gachagua ambaye alimsaidia kutwaa mamlaka kwa kushawishi wakazi wa Mlima Kenya kumpigia kura.

“Kiongozi wa nchi alinyamaza Gachagua “akikaangwa” katika Bunge la Kitaifa na Seneti, hatuna furaha kama wapiga kura kutoka Kirinyaga,” akasema Bw Julius Waweru.

Walimshutumu Dkt Ruto kwa kwenda kinyume na ahadi yake.’ Dkt Ruto aliahidi kwamba hatamdhulumu Naibu wake lakini tulishangaa alipoanza kumdharau hadi kuondolewa kwake kukaidhinishwa na Seneti,’ aliyekuwa MCA, Pius Njogu alisema.

Nyeri

Hali ilikuwa tulivu katika Kaunti ya Nyeri huku wakazi wakiendelea na shughuli zao kama kawaida ila walikuwa na ghadhabu.

Waliozungumza na Taifa Leo wana imani kwamba mahakama itabatilisha uamuzi wa bunge la kitaifa na seneti baada ya mahakama kutoa amri ya kusimamishwa kwa uteuzi wa Prof Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais.

Pwani

Baadhi ya viongozi wa Pwani wamefurahia uteuzi wa Profesa Kithure Kindiki baada ya Bw Rigathi Gachagua kubanduliwa, wakimtaja kama msomi tajika na mchapa kazi.

Spika wa Bunge la Kaunti ya Lamu, Bw Azkhar Mbaraka, alielezea kuridhishwa na uteuzi wa Prof Kindiki kama Naibu wa Rais wa Jamhuri ya Kenya.

“Nimefurahia uteuzi huo, Wakenya sasa wana kiongozi anayefaa kwa nafasi hiyo. Prof Kindiki ni bora kwa nafasi hiyo. Hiyo kazi ilikuwa kubwa sana kwa Bw Rigathi. Ila namtakia afueni ya haraka, na awe na uwezo wa kufanya uamuzi sawa kwa manufaa ya nchi,” akasema Bw Mbarak.

Wakati huo huo, alihimiza viongozi kuwaunganisha Wakenya na sio kuwatenganisha.

Seneta wa Mombasa, Bw Mohamed Faki na mwenzake Miraj Abdallah ambaye ni Seneta Maalum, waliunga uteuzi wa Prof Kindiki, wakieleza kuwa anaweza kumsaidia Rais kuongoza nchi.

“Ningependa kumpongeza sana Prof Kindiki kwa uteuzi. Ni wazi kuwa amefanya kazi yake ya uwaziri kwa weledi hata katika nyakati za maandamano ya kupinga serikali ambapo taifa lilipitia majaribu,” akasema Bi Miraj.

Kwa mujibu wa Seneta huyo, hakuna aliyefurahia kuona Bw Gachagua akiondolewa uongozini kwa kuwa, walikuwa pamoja katika shughuli ya kujitafutia uungwaji mkono katika maeneo mbalimbali nchini.

“Jana (Alhamisi) ilikuwa siku ngumu sana kwa Kenya Kwanza, sioni yeyote aliyefanya kampeni na Dkt Ruto na Gachagua angefurahia kuondolewa kwake uongozini. Hatupaswi kufurahia kuona kiongozi mkubwa akianguka. Tunapaswa kujifunza,” akasema Bi Miraj.

Kwa mujibu wa Bw Faki, Prof Kindiki alifaa sana kwa uteuzi huo. Alieleza kuwa , naibu wa rais mteule amefanya vyema katika wizara ya usalama wa ndani.

“Tuna imani na Kindiki kwa kuwa ni msomi.Ninamtakia kila la kheri katika kazi yake mpya,” akasema Bw Faki.

Mbunge wa Kaloleni Bw Paul Katana pia alimpongeza Prof Kindiki akihoji kuwa, wakati wa kutumikia wananchi ulikuwa umefika na anapaswa kufanya hivyo akichukua wadhifa huo.

“Naunga mkono uteuzi wake kwa sababu Rais ana imani naye katika kufanya kazi yake. Tumeona kuwa amekuwa akijitahidi kutatua shida za Wakenya. Hata kule Kaloleni alikuja na kuwasaidia watu wakati kulikuwa na kiangazi. Nampongeza nikisema tutamuunga mkono ili tuhakikishe anatimiza malengo atakayokuwa nayo kama naibu wa Rais,” akasema Bw Katana.

Taarifa ya George Munene, Kalume Kazungu, Wachira Mwangi na Labaan Shabaan