Wakenya 142 kutuzwa Mashujaa Dei Kwale
WAKENYA 142 watatambuliwa na kutuzwa Jumapili katika maadhimisho ya Mashujaa Dei kutokana na wajibu muhimu waliotekeleza katika kukuza maendeleo.
Kamishna wa Mkoa wa Pwani, Rhoda Onyancha, alisema kuwa wale watakaotunukiwa tuzo wameteuliwa kutoka kila kaunti na tayari wamewasili Kwale kwa ajili ya sherehe hizo.
Sherehe hizo zinaandaliwa kwa mara ya kwanza katika Kaunti ya Kwale ambapo Rais William Ruto ataongoza taifa.“Mashujaa watakaotambuliwa katika hafla hii ya kila mwaka tayari wamefika Kwale. Wameteuliwa kutoka kila kaunti nchini,” alisema Bi Onyancha.
Alikuwa akizungumza wakati wa kikao na wanahabari kilichofanyika katika hoteli ya Jacaranda Indian Ocean Beach Resort huko Diani, Kaunti ya Kwale, ambapo Katibu wa Utangazaji Edward Kisiangani, Msemaji wa Serikali Issac Mwaura, Naibu wake Mwanaisha Chidzuga, na Kamishna wa Kaunti ya Kwale Stephen Orinde walihudhuria.
Bi Onyancha alisema serikali imejitahidi kuweka miundomsingi mbalimbali katika eneo la Pwani.
Pia alisema matukio hayo tayari yameimarisha uchumi wa Kaunti ya Kwale, na kuhimiza wageni waliopo kwenye hafla hiyo kuchunguza vivutio vingine vya utalii.
“Kwale pia ni eneo lenye vivutio vingi vya kitalii. Baada ya sherehe, hamna haja ya kurudi nyumbani mara moja. Mnaweza kutembelea maeneo kama misitu ya Kaya kujifunza kuhusu utamaduni, pia kuna fukwe na Mbuga ya Wanyama ya Shimba Hills,” alisema Bi Onyancha.
Aliongeza kuwa maafisa wa usalama wameweka mikakati kuhakikisha kuwa kuna mtiririko mzuri wa magari kati ya Mombasa na Lunga Lunga kabla na baada ya hafla hiyo.
Washiriki wa hafla hiyo watatumia milango miwili kuingia Uwanja wa Kwale mjini Kwale, ambao ndio mwenyeji wa sherehe.
Bado haijabainika ikiwa aliyekuwa naibu wa Rais Rigathi Gachagua atahudhuria hafla hiyo au la.
Maandalizi yalifika kilele mapema mwezi huu ambapo mbali na miradi kukamilishwa, miji kama Kwale na Diani imepata sura mpya.
Ujenzi wa Uwanja wa Kwale wenye uwezo wa kuchukua watu 10,000 umebadilisha mandhari ya mji wa Kwale, huku barabara kadhaa zikiboreshwa na kuimarisha kaunti hiyo.
Huko Diani, mapambo mbalimbali yamewekwa kwenye barabara. Barabara kuu pia imejengwa inayounganisha Uwanja wa Ndege wa Diani na Barabara ya Beach kwa urahisi wa wale wanaotua Diani.
Ndege, hoteli na vituo vya malazi vimejaa kutokana na idadi kubwa ya watu wanaosafiri kuja Kaunti ya Kwale kushiriki sherehe za Mashujaa Day.“Mbali na Mashujaa, ni msimu wa kilele na kuna shughuli nyingi zinazovutia wageni,” alisema Katibu wa Utalii John Ololtuaa.
Alieleza kuwa miundombinu mbalimbali kama upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Diani imechangia pakubwa katika kukuza sekta ya utalii nchini.
Aliongeza kuwa Jumatatu ikiwa ni sikukuu, Wakenya wanapaswa kufurahia fursa za burudani, hasa katika Fukwe ya Diani ambayo imetajwa kuwa fukwe bora barani Afrika katika Tuzo za World Travel.
Jumatano wiki hii, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) Charles Kahariri aliongoza majeshi katika mazoezi ya maandalizi kuelekea siku ya sherehe.