Michezo

Ingwe wajinyanyua KPL

January 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA CECIL ODONGO

AFC Leopards Alhamisi waliandikisha ushindi wao wa pili kwenye ligi kwa kuicharaza Chemelil Sugar 2-1 katika uga wa Moi jijini Kisumu.

Ingwe walifungua ukurasa wa mabao katika kipindi cha kwanza Jaffery Owiti alipotumia kutoelewana vyema kwa kipa wa Chemelil Sugar Kevin Otieno na mlinzi Crispin Opondo kufunga bao safi baada ya kupata mpira kirahisi.

Bao hilo muhimu lilipatikana baada ya Ingwe kuwazidishia wapinzani presha kwa kumiliki asilimia kubwa ya mpira na kukita kambi kwenye lango lao wakilenga kufunga goli.

Hata hivyo, kiungo mahiri wa Ingwe Eugene Mukangula alitia msumari moto kwenye kidonda cha Chemelil katika mwanzo wa kipindi cha pili kwa kufunga bao la pili.

Juhudi za kocha wa Chemelil Francis Baraza kuongeza makali ya safu yake ya ushambulizi kwa kumleta Felix Oluoch na kumwondoa uwanjani Tindi Biko hata hivyo zilionekana kuongeza nguvu wenyeji hao.

Juhudi hizo zilizaa matunda katika dakika ya 75 ChemeliL Sugar walipopewa penalti baada ya winga wa AFC Leopards Robinson Kamura kushika mpira katika eneo la hatari.

Hata hivyo, Ingwe walishikilia uongozi wao hadi mwisho wa mechi kwa kuwaingiza madifenda Dennis Shikayi na kumwondoa starika Marcelo Kahez ili kuzima mashambulizi ya Chemelil.

Ushindi huo ulimpa nafuu kocha Marko Vesiljevic ambaye amekuwa akishtumiwa na mashabiki kwa kutoongoza timu vizuri ili kutwaa ushindi.