Maoni

MAONI: Masaibu ya Gachagua yanatokana na ulimbukeni wa kisiasa

Na BENSON MATHEKA October 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MASAIBU ya Naibu Rais aliyetimuliwa mamlakani Rigathi Gachagua yanatokana na ulimbukeni wa siasa.

Anaonekana kutofahamu kuwa wanasiasa huwa wanajali maslahi yao na hakuna wakati hata mmoja wanahurumia yeyote wanayeshuku kuwa, bila hata kuthibitisha, anahatarisha maslahi yao.

Hakuna wakati hata mmoja ambao mwanasiasa huwa na maslahi ya washirika wake au ya wapigakura katika moyo wake. Wanachofanya wanasiasa ni kutumia wenzao na wapiga kura kutimiza malengo yao binafsi.

Wanasiasa huwa pia wanatumiana kutimiza maslahi yao hasa wanaposaka nyadhifa za kitaifa ukiwemo urais kwa kurai wenzao walio na ushawishi au wanaotoka maeneo yaliyo na idadi kubwa ya wapiga kura kuwawezesha kushinda wapinzani wao na kutwaa mamlaka.

Hali huwa inabadilika wakishinda na kuingia mamlakani. Ukuraba wa kisiasa ambao wanasiasa huwa nao wakati wa kampeni huwa unaisha na nafasi yake kuchukuliwa na utiifu na uaminifu.

Hakuna anayeshinda kiti cha kisiasa anayeweza kuvumilia mtu aliyemsaidia akihisi kuwa anapungua kwa utiifu na uaminifu, anatishia wadhifa wake au anakuwa kizingiti kwa maslahi yake.

Hii ndiyo hufanya wanasiasa walioonekana kuwa marafiki wakubwa wakati wa kampeni kubadilika na kuwa mahasimu wakubwa wakiingia mamlakani na waliochukuliwa kuwa maadui wa dhati wakisaka uongozi kuungana na kuwa washirika baada ya uchaguzi.

Haya ni mafunzo ambayo kila anayeazimia kuwa mwanasiasa anafaa kukumbatia na kuweka kwa moyo.

Ni mafunzo ambayo Bw Gachagua anaonekana hakupata kwa miaka mitano ambayo alikuwa mbunge kiasi cha kutolinda maslahi yake kupitia mkataba wa maelewano na Rais William Ruto.

Ni hulka inaweza tu kuhusishwa na ulimbukeni wa siasa na ambayo kwa sasa imemtumbikiza katika majuto.