Jinsi eneo la Bonde la Ufa limegeuzwa kitovu cha bidhaa feki nchini
MAKACHERO kutoka Idara ya Upelelezi Nchini (DCI) wameanzisha operesheni ya kuwakamata wakora ambao wamekuwa wakitengeneza na kuuza bidhaa ghushi katika ukanda wa Kusini mwa Bonde la Ufa.
Hii ni kufuatia ufichuzi kuwa wafanyabiashara wakora wamegeuza ukanda huo pahala pa kuuza bidhaa feki na kuwacha watengenezaji bidhaa halali na serikali wakipata hasara kubwa.
Makachero wa DCI, maafisa kutoka Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) na Shirika la Kupambana na Bidhaa Ghushi wametwaa pombe na mbegu bandia katika miji mbalimbali ukanda wa Kusini mwa Bonde la Ufa.
Oparesheni hiyo imefichua biashara iliyoshamiri ya bidhaa ghushi ambazo serikali sasa inalenga kutokomeza. Mnamo Oktoba 11, washukiwa watatu walikamatwa kwenye oparesheni iliyolenga kutokomez kujaa kwa bidhaa ghushi hasa pombe feki jijini Nakuru na maeneo ya karibu.
Maafisa kutoka DCI, Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu ya Kaunti Nakuru na KRA, walivamia eneo ambalo pombe feki imekuwa ikipakiwa katika barabara ya Print Press, Industrial Area, Nakuru.
Mitungi miwili unusu ya kemikali aina ya ethanol, mashine ya plastiki na magunia 60 yenye chupa za kupakia pombe yalipatikana. Pia nembo ya kupachika kwenye chupa kuonyesha brandi maarufu za pombe ili kuwahadaa wateja pia zilipatikana.
“Lazima tutahakikishe kuwa tunaondoa bidhaa feki sokoni na tunatoa wito kwa umma uwe ange na kupiga ripoti kuhusu wanaotengeneza na kuuza bidhaa feki,” akasema Mkuu wa DCI Mohamed Amin.
“DCI itashirikiana na washikadau mbalimbali kuzuia kuenea kwa bidhaa feki sokoni,” akaongeza Bw Amin.
Waliokamatwa Mary Mugure, Peter Macharia na Vincent Kibagendi wamekuwa wakiendesha oparesheni ya kutengeneza na kupakia pombe feki kwa kutumia nembo za pombe maarufu.
Katika tukio jingine mnamo Mei 11, makachero wa DCI wakishirikiana na maafisa wa KRA walipata boxsi 120 zenye pakiti za pombe haramu ambazo ziliwekewa muhuri bandia za KRA katika eneo la Pipeline jijini Nakuru.
Thamani ya bidhaa zote ambazo zilinaswa zilikadiriwa kuwa Sh730,000 huku KRA ikikadiria ilipata hasara ya ushuru wa Sh342, 482.
Mnamo Machi 20, maafisa wa DCI nao walipata mbegu feki za thamani ya Sh12 milioni wakati walivamia kampuni moja ambayo ilisajiliwa kama ya kuhifadhi mbao.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya kukagua mbegu kwenye Shirika la Kutathmini na Kukagua Mimea (KEPHIS) Simon Maina alisema kuwa watu watatu wamekamatwa kuhusiana na kuuzwa kwa mbegu feki ukanda wa kusini mwa Bonde la Ufa.
Wakulima kutoka Nakuru, Bomet, Narok, Kericho na Nyandarua wamekuwa wakilalamikia mbegu feki kujaa sokoni.
“Nakuru na maeneo mengine Kusini mwa Bonde la Ufa ndiko kitovu cha kilimo nchini. Kuna wafanyabiashara wakora ambao wanatumia hilo na kuwahadaa wakulima kwa kuwauzia mbegu feki hasa wakati wa upanzi,” akasema Bw Maina.