Mtihani kwa majaji kuamua iwapo Gachagua ataponea au atazama kabisa na kusahaulika
NAIBU Rais aliyeng’atuliwa mamlakani Rigathi Gachagua leo Jumanne atafahamu iwapo atapoteza wadhifa huo kabisa, mahakama ikitarajiwa kutoa uamuzi iwapo itaruhusu Profesa Kithure Kindiki kuapishwa kama naibu rais.
Bunge la Kitaifa na Mwanasheria Mkuu waliwasilisha kesi Ijumaa iliyopita ya kutaka amri itolewe ili Profesa Kindiki aapishwe kama naibu rais.
Katika kile ambacho kimewakoroga nyongo mawakili wa Bw Gachagua na kuibua maswali mengi, kesi hiyo ilisikizwa mnamo Jumamosi.
Hii ni baada ya Bw Gachagua kuondolewa mamlakani kutokana na hoja iliyopitishwa na Bunge la Kitaifa pamoja na ikadumishwa na ile ya Seneti.
Iwapo uamuzi utatolewa wa kuondoa amri inayozuia kuapishwa kwa Profesa Kindiki basi Bw Gachagua atakuwa amepoteza rasmi wadhifa huo.
Haya yanafanyika wakati ambapo Gachagua jana aliandikia Idara ya Mahakama akihoji ni vipi moja kati ya kesi zilizopinga kutimuliwa kwake iliwasilishwa mbele ya jopokazi la majaji watatu pasipo idhini ya moja kwa moja kutoka kwa Jaji Mkuu Martha Koome.
Kupitia barua aliyoandikia naibu msajili wa Mahakama Kuu, Bw Gachagua alishangazwa na jinsi jopokazi hilo, lililokuwa limebuniwa awali na Jaji Mkuu Koome, ‘lilikusanyika upesi’ Jumamosi iliyopita kusikiza kesi iliyolenga kutupilia mbali agizo la kuzuia kuapishwa Profesa Kindiki.
Bw Gachagua, kupitia wakili wake John Njomo, alisema “kasi ya ajabu” kwenye namna ambavyo majaji Eric Ogola, Anthony Mrima na Freda Mugambi waliangazia na kutoa mwongozo wa kusikizwa hii leo Jumanne, Oktoba 22, 2024 kwa kesi zilizowasilishwa katika Mahakama Kuu ya Nairobi na nyingine Kerugoya.
Wakili alisema yamkini “kuna njama zilizopangwa vyema vya kupuuzilia mbali haki za mlalamishi” kwa kumnyima mchakato wa haki wa kusikizwa kuanzia bunge la kitaifa, seneti na sasa katika Idara ya Mahakama.
“Huku tukisubiri, tuliagizwa kuwa uchunguzi uanzishwe ili kubaini jinsi (Kesi Nambari E565 ya 2024 katika Mahakama Kuu ya Nairobi) ilivyosonga kutoka kwa Jaji Chacha hadi kwa majaji hao watatu bila maelekezo ya moja kwa moja kutoka kwa Jaji Mkuu,” alisema.
Jaji Mwita alisitisha mipango ya kuziba pengo lililoachwa na Bw Gachagua kama Naibu Rais hadi Oktoba 24 wakati kesi hiyo itakapotajwa mbele ya jopokazi la majaji walioteuliwa na Jaji Mkuu Koome.
Mjini Kerugoya, Jaji Mwongo aliruhusu ombi sawa na hilo katika kesi iliyowasilishwa na David Mathenge, Peter Gichobi, Grace Muthoni, Clement Muchiri na Edwin Munene, na kuagiza vilevile kesi hiyo itajwe Oktoba 24.
Lilipoelekea mahakamani, Bunge lilihoji kuwa japo kesi zilizowasilishwa zilikuwa zimepitwa na wakati, zinasheheni athari kuu zinazoweza kuhujumu maslahi ya umma kwa kuwa BwGachagua alikuwa tayari amebanduliwa kama naibu rais ilhali korti ilisimamisha Profesa Kindiki kutwikwa wadhifa huo.
“Mlalamishi (Bunge la Kitaifa) anahofia kuwa iwapo kesi hii haitashughulikiwa upesi na maagizo yanayofaa kutolewa, nchi itatumbukia katika changamoto kuu kikatiba na umuhimu wote wa ombi hili utaambulia patupu,” alisema Bw Eric Gumbo katika wasilisho hilo.
Kesi hiyo iliwasilishwa mbele ya majaji watatu Oktoba 19 walioagiza suala hilo litajwe hii leo ili maelekezo zaidi yatolewe.
“Kwamba kutokana na hali ya dharura ya suala hili na uzito wa masuala yaliyomo, tunaagiza nakala za korti zikabidhiwe washtakiwa ili kuanza vikao vya kusikiza pande husika Jumanne Oktoba 22 saa tano asubuhi katika korti wazi,” walisema majaji.
Katika barua hiyo, Bw Njomo alisema kuna ishara za mwanzo kuwa Jaji Mkuu Koome hata hakuwemo nchini wakati huo.
“Masharti kuhusu mchakato wa kusikizwa kwa njia ya haki unasema kuwa haki haipaswi tu kutendwa, ni sharti ionekane kutendwa. Kinyume na suala lililopo kwa sasa, kuna kisa cha ubaguzi bayana katika namna ambavyo Mlalamishi anatendewa,” anaeleza.
Wakili alisema pia ni dhahiri mamlaka ya Jaji Mkuu yanatekwa kwa njia haramu.
Anasema japo hawakufahamishwa kuhusu kubuniwa kwa jopokazi, walipokezwa maagizo yaliyotolewa na majaji watatu wa jopokazi hilo.
Alisema wanafahamu vyema kuwa jopokazi lilo hilo lilibuniwa kusikiza kesi nyinginezo sita zilizojumuishwa na wala sio kesi hizo mbili zilizowasilishwa Milimani na Kerugoya.
Alirejelea jinsi jopokazi hilo, lilipokuwa likitupilia mbali ombi la kusimamisha mchakato wa ufurushaji, lilikataa vilevile ombi la Bw Gachagua la kumsogeshea karibu tarehe ya kusikizwa kwa kesi yake na kusisitiza tarehe iliyokaribu zaidi inayoweza kupatikana ni Oktoba 29.