Habari za Kitaifa

Mwinjilisti aliyesaidia kuchaguliwa kwa Ruto amgeuka baada ya Gachagua kutemwa

Na KEVIN CHERUIYOT October 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MWASISI wa Kanisa la Faith Evangelistic Ministries (FEM) Mwinjilisti Teresia Wairimu amevutia hisia mseto kufuatia mahubiri yake yenye utata wikendi yaliyokosoa utawala wa Rais William Ruto.

Mwinjilisi Wairimu, ambaye ni rafiki wa muda mrefu wa Mama Taifa Rachel Ruto, yamkini amepoteza imani na serikali ya Kenya Kwanza.

Katika mahubiri yake, alisema kanisa lilikuwa na uhakika kwamba lilifanya uamuzi mwafaka kwa kumpigia kura Rais Ruto, lakini sasa hali imebadilika.

“Najua wengi wetu tulikuwa tunatazama televisheni. Tuliaibika mno,” alisema Mwinjilisti Wairimu.

Alisema badala ya wabunge kuangazia masuala yatakayosaidia taifa kukua kiuchumi, waliamua kujadili kuhusu kumfurusha Naibu Rais pasipo kuwapa fursa ya kusema lolote.

Kutimuliwa kwa Bw Gachagua kumeharibu ukuruba wake na Rais na familia yake akisema hatampigia kura katika uchaguzi ujao bila umakinifu.

“Kama mpiga kura, nimeaibika. Katika uchaguzi ujao ni sharti unishawishi vya kutosha. Tumechoshwa na kelele. Tunataka watekelezaji, tunataka wafanyakazi.”

Mwinjilisti huyo alimhimiza Rais kuhudumia nchi na watu waliomchagua na wala sio kuwapiga vita.

Aidha, aliwaonya viongozi waliochaguliwa kuwa huenda wakafurushwa na Wakenya katika uchaguzi ujao ikiwa hawatafanya kazi yao kama wabunge.

Katika maombi yake, Mwinjilisti Wairimu alimsihi Mungu ang’oe uovu nchini na viongozi wafisadi akisema Wakenya walipiga kura ili wapate amani sio vita.

Japo mahubiri hayo yamejiri baada ya Bw Gachagua kutimuliwa, yameibua masuali kuhusu ushawishi wa kanisa katika kufanya maamuzi.

Mwinjilisti Wairimu amekuwa rafiki wa karibu wa familia ya Rais Ruto, urafiki ulioanzia 2012 na ni mwandani wa karibu zaidi wa Pasta Dorcas Gachagua, ambaye wamehubiri pamoja kwa muda mrefu vilevile.

Katika ibada ya kutoa wakfu ikulu baada ya ushindi wa Kenya Kwanza 2022, Mwinjilisti Wairimu alimfananisha Rais Ruto na mhusika katika Biblia anayefahamika kama Daudi, aliyeinuka kutoka kulisha kondoo wa baba yake na kuwa moja kati ya wafalme tajika wa Israeli.

Hapa, alimfananisha rais na Daudi maadamu Dkt Ruto amekuwa akidai kuwa hasla wa kweli na mtoto wa maskini katika ulimwengu unaotawaliwa na mabwenyenye kabla ya kuinuka kuwa rais.