Makala

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Ya Rabi tujaalie subira na hekima wakati huu mgumu

Na ALI HASSAN October 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo. Tumejaaliwa siku nyingine bora na tukufu kuambizana na kukumbushana kuihusu dini yetu tukufu ya Kiislamu.

Ama kabla ya kujitoma kwenye mada ya leo, tuchukue uzito wa nafasi hii kumshukuru, kumhimidi na kumpwekesha Muumba wetu, Allah (SWT). Katika uzi uo huo wa ufunguzi, tumtakie kila la kheri na dua Mtume wetu (SAW).

Dua na maombi yetu pia yawaendee ndugu zetu kote duniani ambao wanakabiliwa na jakamoyo la mauti na khofu ya uvamizi. Mashambulizi na mavamizi ambayo yanashuhudiwa katika ukanda wa Gaza.

Zaidi ya Wapalestina arobaine na wawili alfu wameuawa Gaza. Majeruhi ni wengi mno! Israel ipo katika vuta n’kuvute, iliyopo baina ya Israel na Lebanon, Iran na Gaza. Hali hii imeleta wahka duniani. Subhanallah!

Aidha, nchi kama Urusi na Ukraine zingali katika panda-shuka na mabomu na mauaji.

Bara la Afrika halijasazwa. Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Sudan, kutaja tu baadhi ya mataifa ya Afrika, kunashuhudiwa purukushani.

Je, mauaji haya hayakugusi mshipa mja mwenzangu? Je, ulimwengu na walimwengu wake, tutamwambia nini Mwenyezi Mungu siku ya mwisho?

Ama kwa hakika ni wajibu wetu, mimi na wewe, kusema kwa ulimi, mdomo, maandishi, mkono na kwa hli yoyote ile kulaani mauaji haya na ugomvi uliokithiri duniani.

Ama kwa hakika tunamlilia Mola wetu kutujaalia subira na hekima katika maisha yetu leo hii. Mbona nasema hivi?

Hadi tunapoyaandika makala haya, kesi mbali mbali zilikuwa zikisikilizwa mahakamani kuhusu kuenguliwa mamlakani Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Kivyovyote vile maamuzi yatakavyokuwa, nchi hii haitokuwa kama ilivyokuwa aswilani. Pameinga mdudu wa suitafahamu baina ya Rais na naibu wake.

Ndio tukasema hapo kabla kuwa maamuzi yatakavyokuwa na yawe.

Lakini maswali ambayo kwamba waja wamesalia nayo vinywani ni kwa namna gani haki ilitendeka?

Ni kwa vipi waja, wananchi, wanaonesha subira, stahamala na uvumilivu.

Familia za wahusika kwenye mchakato mzima huu wa kesi hizi, iwe ni familia ya waliobanduliwa, aila za mawakili, ndugu na jamaa za majaji na wahusika walio kwenye mstari wa mbele, na waja wote, tunahitaji kusameheana, kuvumiliana, na kuwa na subira.

Wanasema watu kuwa haki huleta maridhiano na subira. Je, ni kwa namnA gani haki imeonekana kutendeka kwenye mchakato mzima wa kesi hizi? Iwe kheri In Shaa Allah. Jumaa Mubarak.

[email protected]