Habari Mseto

Mahakama yafungua sehemu ya bweni Endarasha kwa watahiniwa wa KPSEA

Na MERCY MWENDE October 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MAHAKAMA Kuu ya Nyeri imefungua sehemu ya bweni katika shule ya Hillside Endarasha kwa watahiniwa 24 wa mtihani wa kitaifa wa Gredi ya Sita (Kpsea) ambao unatazamiwa kufanywa wiki ijayo.

Katika maagizo yaliyotolewa Alhamisi Oktoba 24 na Jaji Magare Kizito, mahakama iliwaruhusu watahiniwa hao kuingia shuleni na kujiunga na wenzao 57 wa Kpsea, ambao watafanya mtihani.

Jaji huyo alieleza kuwa aliondoa maagizo ya awali yaliyotolewa na mahakama mnamo Oktoba 17, ambayo yalisimamisha kufunguliwa kwa bweni hilo huku ikisubiri ripoti ya afya na usalama kutoka kwa Wizara ya Elimu kuhusu hali ya taasisi hiyo.

Awali Jaji Kizito alikuwa ameagiza wizara kupitia Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti Jane Njogu, kukagua shule hiyo kibinafsi na kuandaa ripoti kuhusu viwango vya usalama.

Hata hivyo, wakati wa kikao cha mahakama Alhamisi, wakili wa Mwanasheria Mkuu Mumbi Kiarie, ambaye anawakilisha Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti, Bodi ya Elimu ya Kaunti, Waziri wa Elimu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kesi hiyo, alisema alipokea ripoti hiyo akiwa amechelewa.

“Sijapata muda wa kuhakiki ripoti hiyo kwa kina kwa sababu ilitumwa kwangu mwendo wa saa tisa jioni Jumatano. Ninaomba muda zaidi wa kuipitia na kuthibitisha utiifu wa maagizo yako,” alisema.

Wamiliki wa shule hiyo David Kinyua, Mary Wanjeri na Bodi ya Usimamizi waliambia mahakama kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Kawi na Petroli ilikamilisha uwekaji umeme kama ilivyoagizwa na Mahakama hapo awali.