Makala

Sheria: Njia ya kudai mali iliyomilikiwa na mume au mke wako kabla ya ndoa

Na BENSON MATHEKA October 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MALI yoyote ambayo inamilikiwa na wanandoa kabla ya ndoa haitambuliwi kama ya ndoa.

Hata hivyo,  kulingana na  Sheria ya Mali ya Ndoa ya Kenya, mtu anaweza kunufaika na mali iliyomilikiwa na mume au mkewe kabla ya ndoa kwa kuchangia kuikuza.

Kwa upande mwingine, mali yoyote ambayo hupatikana wakati wa ndoa ambayo imesajiliwa kwa jina la mwanandoa mmoja, kuna dhana inayoweza kupingwa kwamba mali hiyo inahifadhiwa kama amana kwa mume au mkewe  kwa mujibu wa Kifungu cha 14 cha Sheria.

Dhana hii inaweza kupingwa pale ambapo ushahidi unawasilishwa mbele ya mahakama kuthibitisha vinginevyo.

Ni kwa sababu hii ambapo idhini ya mume au mke inahitajika kabla ya mali ya mtu yeyote aliyefunga ndoa kuhamishwa kwa kuuzwa au kupeanwa kama zawadi na hata kukodishwa.

Idhini hii kwa ujumla inafaa kuthibitisha  kwamba mume au mke anafahamu kuwepo kwa mali hiyo, anafahamu kuwa mali hiyo imesajiliwa kwa jina la mume au mkewe anafahamu shughuli itakayofanyika na kwamba wamekubaliana hivyo; na kwamba amepata ushauri huru wa kisheria na anaelewa maana ya kutoa kibali kwa mujibu wa masharti ya Sheria.

Licha ya haya, wanandoa wanaweza pia kuchagua kuingia katika makubaliano ya kabla ya ndoa ili kusaidia katika kuamua haki zao za kumiliki mali.

Makubaliano kama haya ni halali japo mahakama inaweza kuyaweka kando ikithibitishwa yalifanywa kwa kulazimishwa, ulaghai au hayakidhi masharti ya Kifungu cha 6(4) cha Sheria ya Mali ya Ndoa.

Kwa hivyo, kabla ya kuingia katika makubaliano kama haya, wahusika wanapaswa kushirikisha mawakili ili kutoa ushauri wa kisheria kuhakikisha kwamba ndoa inapovunjika mahakama inaweza kuyazingatia na kutekeleza masharti  hayo. Makubaliano hayo, huwa ni nyenzo madhubuti katika usimamizi wa mali iwapo masharti yataandaliwa kwa haki na kuwe na uwazi kamili kutoka kwa wahusika.

Sheria pia inatoa haki ya kumiliki mali katika ndoa za wake wengi chini ya Kifungu  8 cha sheria ya Mali ya Ndoa ambapo kwa ujumla, kanuni zilizotajwa hapo juu bado zinatumika.

Mali ya ndoa iliyopatikana na mwanamume na mke wake wa kwanza haiwezi kudaiwa na mke wa pili. Hii ni ikiwa mume alipata mali hiyo kabla ya kuoa mke wa pili. Kwa ndoa zinazofanyika chini ya sheria za Kiislamu, masuala yote yanayohusiana na mali ya ndoa yanasimamiwa na masharti ya sheria ya Kiislamu.