Habari za Kitaifa

Kilio SHIF ikifyeka mishahara bila huruma

Na ANGELA OKETCH October 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAKENYA wameelezea masikitiko yao kuhusu makato ya kwanza ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIF) kutoka kwa mishahara yao mwezi huu, huku wagonjwa wakiendelea kukumbwa na changamoto si haba za kupata huduma katika mfumo huo mpya.

Wale ambao wamepokea taarifa zao za mshahara katika siku chache zilizopita wameingia kwenye mitandao ya kijamii, wakitaja athari za makato hayo kwa mipango yao ya kifedha.

Majukwaa ya mitandao ya kijamii na vikundi vya majadiliano kazini vimejaa wananchi wakielezea kufadhaika kwa kile wanachoona kama kupungua pakubwa kwa pesa wanazobakishiwa katika mshahara.

Tangu mpango wa SHIF uanze kutumika Oktoba 1 2024 umekuwa ukichunguzwa vikali huku baadhi ya changamoto zikianikwa na watu wakitilia shaka iwapo watapata faida chini ya hazina hiyo.

Ingawa serikali imetetea SHIF kama suluhisho la muda mrefu la kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya na uwezo wa kuzimudu, Wakenya hawana uhakika nao.

Chini ya NHIF ambayo sasa haitumiki, kiwango cha juu cha mchango kilikuwa Sh1,700.

Hata hivyo, watu binafsi sasa wanatakiwa kuchangia asilimia 2.75 ya mapato ya familia zao, ongezeko kubwa ambalo linabana mshahara ambao tayari umepungua.

Wafanyakazi wengi wanahisi kuwa makato hayo ni ghali bila hakikisho la wazi la huduma bora za afya.

Annastia Akinyi, mzazi aliyezungumza na Taifa Leo, alisimulia jinsi wazazi wenye watoto wenye ulemavu mbalimbali wanavyolazimika kulipa fedha taslimu kununua dawa ilhali wanakatwa kiasi kikubwa cha fedha.

“Inasikitisha sana. Dawa nyingi za watoto wenye ulemavu hazipatikani chini ya bima hii. Unalipa pesa taslimu. Sasa unapoona makato hayo ya SHIF unashangaa jinsi wanavyotarajia watu wanaohitaji dawa hizi wazipate wakienda na pesa zote,” Bi Akinyi alisema.

Alisema SHA imeanza kutekelezwa huku mshahara wake wa Oktoba ukikatwa kiasi kikubwa.

‘Kiasi hiki ni zaidi ya nusu ya kile ninachotumia kwa dawa muhimu ya binti yangu ambayo lazima anywe kila siku na hailipiwi na bima. Tupataje dawa sasa?” aliuliza.

Aliongeza: ‘Tunahitaji kuelezwa jinsi tutakavyopata dawa kila siku, jinsi tunavyokatwa kiasi kama hicho ilhali watoto wetu hawawezi kupata dawa muhimu, pesa hizo zilitosha kulipia dawa zake,’ alilalamika.

Bi Pheobe Ongadi, Mkurugenzi Mtendaji, Mashirika yanayohusika na Saratani Kenya, aliambia Taifa Leo kuwa wakati SHIF ilipozinduliwa, wagonjwa walikuwa na matarajio makubwa kwamba kungekuwa na faida kubwa. Walakini, hadi sasa imekuwa ya kukatisha tamaa.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Taasisi ya Kitaifa ya Saratani, Dkt Elias Melly, alisema wanatambua kuwa kuna changamoto kwa sababu haiwezi kutatua tatizo ambalo wagonjwa wanalishuhudia hivi sasa.