Makala

Uhuru kujitokeza hadharani kwatoa tumaini ataangazia masaibu ya Gachagua

Na CHARLES WASONGA October 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KUONEKANA hadharani kwa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta Alhamisi, baada ya kukosekana machoni pa umma  tangu Juni mwaka huu, kumepokewa na Wakenya kwa hisia mseto.

Kupitia jumbe kwenye majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii, baadhi yao walimtaka azungumzie matukio mbalimbali nchini, haswa masaibu yanayomzonga Naibu Rais aliyetimuliwa Rigathi Gachagua.

“Wakati ambapo hukuwepo, waliuza uwanja wa JKIA, wakatuletea bima ya SHA ambayo haifanyi kazi kisha wakamtimua Riggy G. Sasa ukirudi kutoka Abidjan, kohoa kidogo tukusikie,” akasema Ken Mwangi kupitia Facebook.

Mnamo Alhamisi, kitengo cha mawasiliano katika afisi ya Bw Kenyatta kilisambaza picha kadhaa mitandaoni zikimwonyesha Bw Kenyatta Kenyatta akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Felix Houphouet Boigny jijini Abdijan, nchini Cote d’Ivoire.

Kulingana na maelezo yaliyoandamanishwa na picha hizo, Bw Kenyatta alitua nchini humo kuhudhuria makala ya 15 ya Mkutano wa Afrika wa kuhimiza Amani, Usalama na Uthabiti.

Mkutano huo ulioandaliwa na Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) unalenga kujadili njia za kuzuia mapigano yanayoshuhudiwa katika mataifa mbalimbali Afrika.

“Sasa mumemuona kiongozi wenu mpendwa akiwa shwari kiafya ni hivi karibuni atazunguka sehemu mbalimbali Kenya,” kulingana na maelezo yaliyoandamanishwa na picha hizo.

Mara ya mwisho Bw Kenyatta kuzungumzia matukio nchini ilikuwa mnamo Juni 25, mwaka huu alipotoa taarifa kuhusu maandamano ya Gen-Z kupinga Mswada wa Fedha wa 2024.

Alituma rambirambi zake kufuatia vifo vilivyotokea kufuatia makabiliano kati ya polisi na waandamanaji akisisitiza kuwa raia wako na haki ya kuandamana na “ni wajibu wa viongozi kusikiza malalamishi yao.”

Uvumi umekuwa ukienezwa kuhusu hali ya afya ya Bw Kenyatta baada yake kutoonekana hadharani, wala kusikika, kwa kupindi cha miezi minne.

Wanasiasa kutoka Mlima Kenya, haswa wandani wa Bw Gachagua, sasa wamejawa na matumaini kuwa huenda Bw Kenyatta akazumguzia masaibu yanayomzonga na kiongozi huyo.

“Tunafurahi kwamba sasa Uhuru amejitokeza na afisa yake imewahakikishia Wakenya kwamba yuko sawa na tumemwona kwenye picha akiwasili nchini Cote d’Ivoire. Kama kiongozi wetu wa Mlima Kenya ni matarajio yetu kwamba hivi karibuni tutasikia sauti yake akitoa kauli kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa likiwemo hili la kudhulumiwa kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua,” anasema Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya.

Kwa upande wake, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Nairobi Joseph Kaguthi Ijumaa alikunuliwa akisema kuwa wanachama wa baraza la wazee wa jamii ya Agikuyu wamekuwa na hamu ya kumfikia Bw Kenyatta kuhusiana na madhila ya Bw Gachagua lakini hawakufanikiwa.

“Kutoonekana kwake kulitupa wasiwasi mwingi. Tulitaka kukutana naye tupate hisia zake kuhusu yale yanayoendelea nchini kwani anatambuliwa kama mwenye usemi mkubwa katika masuala yanayohusiana na jamii yetu,” akanukuliwa akisema.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema hakikisho kutoka kwa afisi ya Bw Kenyatta kwamba yuko shwari na “hivi karibuni atakuwa akizunguka Kenya,” linaashiria kuwa huenda rais huyo mstaafu akaanza kuonekana na kuzungumzia masuala ya kitaifa.

“Kwa kutoa picha za mheshimiwa Uhuru Kenyatta na maelezo kuhusu hali yake ya afya, kwanza afisi yake inalenga kuondoa dukuduku mioyoni mwa Wakenya kwamba hali yake ya afya haikuwa shwari. Pili, afisi hiyo inawajuza Wakenya kwamba kiongozi huyo atarejelea maisha yake ya kawaida na hatachelea kuzungumzia masuala ibuka yenye umuhimu wa kitaifa,” akasema Bw Dismus Mokua.

“Ni wazi kuwa Wakenya watataka kupata hisia zake kuhusu kutimuliwa kwa Bw Gachagua na mpango unaoendelea wa kuweka usimamizi wa asasi za serikali chini ya usimamizi wa kampuni za kibinafsi, haswa ile ya Adani,” anaongeza.