Afya na Jamii

Kundi la ‘Vijana Bora’ linavyohamasisha jamii kubadili mtazamo kuhusu afya ya akili

October 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

KUNDI la vijana kutoka Kaunti ya Kiambu maarufu kama Vijana Bora limejitolea kusaidia kupunguza idadi ya wanaoangamia kutokana na matatizo ya akili.

Kulingana na mkurugenzi wake Mageto Momanyi, kundi hilo lilianzishwa mwaka wa 2022 baada ya kutambua kuwa vijana wengi waliokuwa wakihangaika na masuala ya afya ya akili hawakuwa wakipata msaada waliohitaji.

Kulingana na Bw Mageto, afya ya akili ni kipengee muhimu cha ustawi ila hupuuzwa mara nyingi au kutoeleweka nchini Kenya na nchi nyingine zinazoendelea.

“Katika maeneo yanayoendelea, huduma ya afya ya akili na usaidizi unaweza kuwa mdogo, na hivyo husababisha unyanyapaa na kutoelewana kuhusu ugonjwa wa akili. Kwa sababu hiyo. vijana wengi wanaokabiliana na matatizo ya afya ya akili huenda wasipate msaada wanaohitaji,” anaeleza Momanyi.

Mageto Momanyi akiongoza kundi la Vijana Bora kuhamasisha umma wakati wa siku ya kuzuia kujitoa uhai duniani, Septemba 10, 2024. Picha|Leah Makena

Momanyi anasisitiza kuwa ni muhimu kutambua afya ya akili na hitaji la utunzaji bora wa afya ya kili. Anaongeza kuwa afya ya akili ina jukumu muhimu la jinsi tunavyofikiria, kuhisi, na huathiri tabia zetu na nyanja zote za maisha ya mwanadamu.

“Afya bora ya akili huturuhusu kukabiliana na changamoto za maisha, kuunda na kudumisha uhusiano mzuri na kuishi maisha yenye kuridhisha na yenye tija. Habari mbaya ni kuwa huduma ya afya ya akili na usaidizi unaweza kuwa mdogo. Hii ndio sababu tumejitokeza kufanya juhudi ya kusaidia kadri ya uwezo wetu,” anazidi kueleza Mageto.

Kundi hili la ‘VijanaBora’ ni mahiri kwenye maeneo ya Thika na Kiambu na wameweka miradi kabambe ili kufikia walioathirika na afya ya akili. Mradi wa kwanza ni wa Tujibonge, podikasti ya kila wiki inayolenga kuwezesha akili na maisha yenye kutia moyo kupitia mazungumzo ya wazi na ya uaminifu kuhusu afya ya akili na ustawi. Kila kipindi huangazia mahojiano ya wataalamu, hadithi za kibinafsi na majadiliano ya kina kuhusi mada mbali mbali, kuanzia hali ya kawaida na afya ya akili hadi utafiti na matibabu ya hivi punde.

Mradi mwingine ni ule wa ‘Nyumbani Productions’ ambao ni mpango wa kujifunza unaosaidia vijana na wanajamii kujifunza ustadi wa kupiga picha na kutengeneza filamu huku ukikuza ufahamu wa wanajamii. Kupitia warsha zinazoshirikisha, mihadhara ya wageni na mradi wa kikundi shirikishi, washiriki hujifunza kusimulia hadithi za picha zenye kuvutia na kuchunguza masuala ya kijamii ambayo ni muhimu kwao.

Pia, kundi hili lina mradi wa ‘MamaBora’, programu ya kina iliyoundwa kuwa mwenzi wa uzazi mtandaoni kwa akina mama na walezi. Programu hii inalenga kutoa afikiaji wa papo hapo kwa ushauri na marifa ya kitaalamu na inashughulikia nyanja zote za ukuaji wa mtoto, masuala ya usalama na mada zingine muhimu zinazohusiana na kila hatua ya malezi.

Badhi ya vijana ambao wamenusurika kupitia kundi hili wanakiri kuwa kuna haja ya kuendelea kusaidia wengi wanaozama kwenye unyanyapaa wa ugonjwa wa akili.

Brian Makori, mwathiriwa aliyejaribu kujitoa uhai mara tatu baada ya kukumbwa na tatizo la afya ya akili. Amepata mtazamo mpya wa kimaisha kupitia upigaji picha na muziki. Picha|Leah Makena

Brian Makori ambaye ni mwathirika anasema kuwa vijana wengi hawapati huduma za afya ya akili akiongeza kuwa unyanyapaa na ubaguzi unaweza kuenea dhidi ya watu wenye matatizo y afya ya akili.

“Iwapo suala la utunzaji bora wa akili litashughulikiwa, wengi watafikiwa na unyanyapaa utakomeshwa kwa sababu Wakenya watakuwa na ufahamu wa afya ya akili,” anaeleza Makori.

Brian anashukuru VijanBora kwa wosia wao alipokuwa akipitia hali ngumu katika maisha.

“Ninashukuru VijanaBora kwa kuniokoa kutoka kwenye giza hilo. Nimejaribu kujitoa uhai mara tatu mfululizo bila kufanikiwa. Kwa sasa, ninajishughulisha na upigaji picha na muziki, mambo ambayo yamebadili mtazamo wangu wa maisha,” anasimulia Makori.

Wakati wa Siku ya Afya ya Akili Duniani mapema Oktoba, shirika la afya duniani WHO lilipiga jeki suala hili kwa kutaka kuongezwa kwa ufahamu wa masuala ya afya ya akili na kuhamasishwa kwa juhudi katika kusaidia watu wenye changamoto za akili.

“Kila mwaka, Septemba 10 hutoa fursa ya washikadau wote wanaoshughulikia masuala ya afya ya akili kuzungumza kuhusu kazi zao, na nini zaidi kinapaswa kufanywa ili kufanya huduma ya afya ya akili kuwa jambo la kweli kwa watu duniani kote,” lilisema shirika hilo.

Kwa sasa, VijanaBora wanaendeleza kampeni zao kwenye mitaa mbali mbali hapa nchini na kwenye mitandao ya kijamii huku wakiwataka watu wote haswa vijana kujitokeza kwenye mazungumzo waziwazi iwapo wanakabiliwa na tatizo la afya ya akili.