Sio saa hii: Kaunti zaambiwa zitaarajie pesa baadaye kidogo
MAGAVANA wanahitajika kuwa na subira ili wajue jinsi magatuzi yatagawana mapato kuanzia mwaka ujao, hii ni kufuatia uhaba wa fedha katika Tume ya Ugawaji Mapato (CRA).
Haya yanajiri baada ya CRA kukatwa bajeti ya Sh150 milioni, hali ambayo inaathiri uundaji wa mfumo mpya wa ugavi wa mapato unaofaa kuanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha utakaokamilika Juni 30, 2026.
Bunge la Seneti linafaa kukamilisha mpango huo kufikia Desemba 2024.
Mfumo wa sasa ni wa tatu tangu kuanza kwa ugatuzi 2013 na umetumika tangu July 2020.
Mwenyekiti wa CRA Mary Chebukati anasema kukatwa kwa bajeti (kutoka Sh516 milioni hadi Sh366 milioni) kumechelewesha utekelezaji wa mfumo mpya baada ya Mswada wa Fedha wa 2024 kutupiliwa mbali.
Bi Chebukati anakiri kuwa uhaba wa fedha umeathiri oparesheni za tume hiyo hasaa ushirikishaji wa washikadau.
“Tuliomba kubuni mfumo wa ugavi wa mapato kufikia Julai mwaka huu. Siwezi kuwaambia tutamaliza lini kwa sababu tuna uhaba wa fedha. Tunaratajia kupata rasilimali kutoka kwa Hazina ya Kitaifa,” alisema Bi Chebukati.
“Tunahitaji Sh30 milioni. La sivyo, tutakuwa tukipata mishahara bila kufanya chochote,” aliongeza.
Mchakato wa kuunda mfumo ulianza Aprili 2023 wakati tume hiyo ilitoa notisi kwa umma kualika mawasilisho kuhusu mapendekezo ya mfumo wa nne wa kugawa rasilimali miongoni mwa kaunti.
Kufikia Mei 2024, CRA ilikamilisha msururu wa mashauriano na kaunti. Hii ilikuwa moja ya hatua ya kutengeneza mfumo.
Mfumo pendekezwa unalenga utumizi wa data za hivi punde na zinazotegemewa ili kuwezesha ugawaji mapato kwa usawa kwa kaunti zote 47.
Vipengele muhimu katika mfumo huu ni mgao wa msingi, idadi ya watu, ukubwa wa eneo, kiwango cha umaskini, jumla ya mapato ya kaunti na hali ya barabara.
CRA itahitajika kuwasilisha mfumo kwa Bunge la Seneti ili uangaziwe na kufanyiwa marekebisho kabla ya kuidhinishwa kufikia Desemba 2024.
Maandalizi ya mifumo iliyopita yamekuwa yakiibua hisia mseto huku washikadau wakitoa mapendekezo yanayowanufaisha. Viongozi wa maeneo yenye idadi kubwa ya watu wamekuwa wakipigia debe kipengele ambacho kinajikita katika idadi ya watu maarufu ‘mtu mmoja, shilingi moja.’
Lakini viongozi wa maeneo ambayo yana idadi ndogo ya watu, hasaa maeneo makubwa, wamekuwa wakipinga wenzao huku wakisukuma ugawaji mapato unaojikita katika ukubwa wa eneo.
Imetafsiriwa na Labaan Shabaan