Jamvi La Siasa

Gachagua aingiza serikali kwenye chengachenga nyingi kuchelewesha kufurushwa

Na MARY WANGARI, SAM KIPLAGAT October 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NAIBU Rais aliyetimuliwa Rigathi Gachagua ameonekana kutumia mbinu za kuendelea kuchelewesha mchakato wa kumfurusha kukamilika na kuapishwa kwa mrithi wake, Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki.

Ni karibu wiki tatu sasa tangu Bunge la Kitaifa lilipopitisha hoja iliyowasilishwa na Mbunge wa Kibwezi Mutuse Mwengi, kuhusu kumng’atua mamlakani Naibu Rais.

Siku chache baadaye, hoja hiyo ilipitishwa Seneti kabla ya bunge kuidhinisha jina la Kindiki aliyeteuliwa na Rais William Ruto, kuziba pengo lililoachwa na Bw Gachagua.

Hata hivyo, zaidi ya wiki moja tangu Bw Kindiki alipoidhinishwa, bado anasubiri kuapishwa huku ikizidi kubainika kuwa huenda Wakenya wakasubiri kwa muda zaidi kabla ya kuwa na naibu rais mpya.

Bw Gachagua, kupitia kikosi cha mawakili wake, ameonekana kubuni mbinu mpya kila uchao za kuchelewesha juhudi za kumzima kisiasa.

Yote haya yalianza kujitokeza siku ya pili ya kikao cha Seneti kuhusu kumfurusha Bw Gachagua ambapo mchakato huo ulichukua mkondo usiotarajiwa baada ya Naibu Rais kukosa kujitokeza na kuwaacha maseneta wakiwa wamegubikwa na sintofahamu.

Baadaye, mawakili wake wakiongozwa na Wakili Mkuu Paul Muite walifahamisha Spika wa Seneti Amason Kingi kuwa Bw Gachagua anaugua maumivu makali ya kifua.

Baada ya vuta ni kuvute ya muda, maseneta waliafikiana kuendelea na mchakato huo ambapo kura ya kumtimua Gachagua iliishia kupigwa saa sita kasorobo usiku.

Kabla ya hapo, Bw Gachagua kupitia mawakili wake alikuwa amewasilisha jumla ya kesi 29 katika juhudi za kusimamisha Seneti kusikiza mashtaka yaliyowasilishwa dhidi yake katika hoja ya kumfurusha.

Hata baada ya Bunge la Kitaifa na Seneti kumfurusha, Bw Gachagua aliwasilisha kesi katika Mahakama Kuu ya Kerugoya, Kirinyaga na Milimani, Nairobi akitaka zisimamishe kuapishwa kwa Kindiki.

Katika juhudi za hivi punde, Bw Gachagua jana alifika katika Mahakama ya Rufaa akitaka mchakato wa kumfurusha usimamishwe na kusubiri uamuzi kuhusu kesi aliyowasilisha utolewe.

Kupitia kesi aliyowasilisha katika Mahakama ya Rufaa, Bw Gachagua alisema hakuridhishwa na uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu uliompa mamlaka Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu ya kuteua jopokazi la majaji watakaoamua kesi husika.

“Mlalamishi, hata hivyo, anahoji kuwa uamuzi uliotajwa unajikita katika Unukuzi usiofaa wa Kifungu 165 (4) cha Katiba na vilevile ukiukaji wa vifungu 25, 27, 47, 48, 50 (1) na 260 kwa kuwa Katiba imetwika mamlaka ya kuteua majaji kwa Jaji Mkuu wa Kenya tu hivyo basi, naibu jaji mkuu hana mamlaka ya kufanya hivyo,” anahoji.

Kupitia wakili John Njomo, Bw Gachagua alisema uamuzi uliotolewa na majaji Eric Ogola, Anthony Mrima na Dkt Freda Mugambi, kando na kuegemea unukuzi usio sahihi wa Kifungu 165 (4) cha katiba ulijikita vilevile katika tathmini isiyofaa ya katiba.

Katika uamuzi uliotolewa wiki iliyopita, jopokazi la majaji lilisema wajibu wa kikatiba uliotekelezwa na Jaji Mkuu chini ya Kifungu 165(4) cha Katiba ni wajibu unaoweza kutekelezwa na Naibu Jaji Mkuu kama msimamizi kama Jaji Mkuu hayupo, ili kuhakikisha majukumu ya kikatiba yanaendeshwa bila kukatizwa.

“Kwa maoni yetu, na kwa kuambatana na kanuni ya kuendeleza katika utawala, walioandika Katiba walifanya maksudi kuhakikisha kuwa usimamizi wa majukumu na utekelezaji wa vipengee vya katiba haukatizwi,” walisema majaji.

Bw Njomo alisema majaji walikosea katika ufafanuzi wao wa katiba.

Wakili huyo pia aliwakosoa majaji kwa kukataa kuongeza muda agizo la muda lililozuia pengo lililoachwa na Bw Gachagua kujazwa na Waziri wa Usalama wa Ndani, Kithure Kindiki.

Muda wa agizo hilo ulikamilika Oktoba 24 na juhudi za mawakili wa Bw Gachagua kuomba muda zaidi ziliambulia patupu.

Agizo lingine lililotolewa na Jaji Richard Mwongo katika Mahakama Kuu ya Kerugoya, bado ipo kumaanisha kuwa Profesa Kindiki hawezi akaapishwa hadi kesi dhidi yake itakapoamuliwa.

“Isitoshe, baada ya kutoridhishwa na uamuzi huo, mlalamishi anahoji kuwa amekata rufaa dhidi ya uamuzi wote pamoja na mchakato wa jopokazi husika uliokataa na kutelekeza kuongeza muda maagizo yaliyotajwa kwenye kesi hii,” anaeleza Bw Njomo.

Bw Njomo alisema anahofia kuwa jopokazi litasonga mbele kusikiza na kutoa uamuzi kuhusu kesi inayolenga kufutilia mbali agizo hilo na kuhujumu kesi ya rufaa iliyowasilishwa.

“Mlalamishi anahoji kwamba, iwapo mahakama hii itadumisha mchakato huo kuendeshwa na jopokazi hili na kutoa cheti cha dharura ili kesi hii ipatiwe kipaumbele kusikizwa pamoja na kesi iliyowasilishwa hapa, kesi ya rufaa itatupiliwa mbali kwa kukosa maana,” alihoji Njomo,

Wakati huo vilevile, Jaji wa Mahakama ya Ajira na Leba, Hellen Wasilwa, ameagiza wafanyakazi wote wa Naibu Rais aliyefurushwa, waliokuwa kwenye likizo ya lazima kuwasilisha kandarasi zao kabla ya maelekezo zaidi kutolewa kuhusu kusikizwa kwa suala hilo.

Jaji Wasilwa alisema kandarasi za waajiriwa wote 108 wanaodaiwa kutumwa kwenye likizo ya lazima, kuambatishwa kwenye kesi hiyo.

Aidha, aliagiza washtakiwa wakiwemo Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor na Mkuu wa Huduma ya Umma Felix Koskei kuwasilisha majibu yao katika muda wa siku saba.

Kesi hiyo itatajwa Novemba 13.