TUZOEE JINA? Ruben Amorim akaribia kupewa kazi ya Ten Hag Man U, mechi za Carabao zikisakatwa
MANCHESTER, Uingereza
KLABU ya Manchester United imeanzisha mazungmzo na kocha Ruben Amorim baada ya kumtimua Erik ten Hag kufuatia matokeo duni tangu msimu huu uanze.
Wakati huo huo, michuano ya Carabao Cup inaingia hatua ya raundi ya 16-bora Jumatano usiku huku kukiwa na jumla ya mechi sita katika viwanja mbali nchini hapa.
Amorim anayenoa klabu ya Sporting Lisbon nchini Ureno ameripotiwa kufikiria kuhusu kazi hiyo baada ya klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza kumuorodheshwa kocha huyo mwenye umri wa miaka 39 katika nafasi ya kwanza miongoni mwa wanaofikiriwa kupewa kazi hiyo.
Ten Hag alitimuliwa Jumatatu, miezi minne tu baada ya kusaini mkataba kuurefusha mkataba wake kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Chini ya Ten Hag, Manchester United wameanza msimu huu kwa matokeo ya kuchanganya, lakini kwa sasa kikosi hicho kiko chini ya aliyekuwa mshambuliaji wao matata, Ruud van Nistelrooy kama kaimu kocha hadi mkufunzi mpya atakapoajiriwa.
Huenda vigogo hao wa EPL wakafikia makubaliano na kocha mpya mwishoni mwa wiki, Amorim akiongoza orodha ya makocha hao baada ya mazungumzo ya awali kufaulu.
Nyakati za usakataji soka, Amorim alichezea klabu ya Braga, Benfica na timu ya taifa ya Ureno aliyochezeshwa kwa mara ya kwanza mnamo 2003.
Hatua ya kumfurusha Ten Hag inajiri baada ya United kupoteza mechi ya EPL kwa West Ham United ugenini kwa 2-1.
“Erik ten Hag ameacha kazi kama kocha mkuu. Tunamshukuru kwa kila kitu amefanya wakati akiwa nasi na tunamtakia kila la heri siku za usoni,” ilisoma taarifa kutoka kwa afisi kuu ya Manchester United.
Akiwa na United, Ten Hag ameisaidia kushinda mataji mawili ya Carabao Cup mnamo 2023 na FA Cup mwaka huu baada ya kujiunga na klabu hiyo mnamo 2022.
Katika mechi sita za Carabao Cup, Manchester United chini ya kocha wa mpito, Ruud van Nistelrooy watakuwa nyumbani kukaribisha Leicester City kuanzia 10:45pm, wakati Arsenal wakiwa ugenini kupepetana na Preston inayoshiriki daraja la Championship.
Newcastle United watapata fursa ya kulipiza kisasi watakapoalika Chelsea katika uwanja wa St James’ Park, siku chache tu baada ya kushindwa 2-1 na wapinzani wao katika pambano la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), ugani Stamford Bridge, Jumapili.
Ratiba ya Carabao Cup Jumatano usiku:
Brighton vs Liverpool (Amerika Express Stadium, 10:30pm), Preston vs Arsenal (Deep dale Stadium, 10:45pm), Manchester United vs Leicester City (Old Trafford, 10:45pm), Newcastle United vs Chelsea (St. Peters’ Park, 10:45pm), Aston Villa vs Crystal Palace (Villa Park, 10:45pm), Tottenham Hotspur vs Manchester City (The Hotspur Stadium, 9:15pm).