MAONI: Ruto si Zakayo, wa Biblia alikuwa msikiza ushauri
Rais William Ruto amelinganishwa na Zakayo wa Bibilia Takatifu ambaye alikuwa mtoza ushuru mkuu.
Ruto amehalalisha matumizi ya jina hilo nchini na hata ughaibuni. Katika sherehe za kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani kwa kinywa chake, aliwakumbusha Wakenya kuwa wamuite Zakayo na vinginevyo, ushuru watatoa.
Watu wakasema Zakayo ashuke. Inavyoonekana bado hajashuka na hamna dalili ya kufanya hivyo. Ndiyo sababu nasema huyu si Zakayo, kama ni Zakayo basi ana moyo mgumu kupita yule tunayemjua. Ama pengine aitwe Zakayo Maradufu.
Upo ukweli wa kauli yangu kwa sababu zifuatazo. Awali Wakenya wamelilia Rais kuhusu tozo kuanzia kwa nyumba, bima ya afya, malipo ya uzeeni, ushuru wa ziada kwa bidhaa nyingi miongoni mwa mambo mengine.
Hata katika maandamano yaliyoongozwa na kizazi cha Gen – Z, suala la maisha kuwa magumu liliambatanishwa na mvua ya ushuru wa serikali.
Je, Rais ameonyesha moyo wa unyenyekevu na kuwaambia Wakenya serikali imechukua ushuru mkubwa kutoka kwao kihalali na kwa njia haramu na itawarudishia ilipokosea?
Je, Wakenya watukufu watarejeshewa kilicholiwa na nzige wa ushuru? Hamna! Badala yake serikali imekuwa mahakamani kuhalalisha tozo hizo.
Yule Zakayo wa Bibilia alipomwona Yesu kwa taabu kutokana na kimo chake, Yesu alimhurumia na kumwagiza ashuke.
Zakayo akajitetea na kuomba radhi kwa kuwaibia watu na kujitajirisha. Akawa radhi kurudisha nusu ya mali yake aliyoipata kwa njia haramu.
Yesu akampongeza. Leo hii kuna watu walikatwa tozo za nyumba kabla ya mchakato wa sheria kufuatwa.
Pamoja na kesi kusikizwa na kuamuliwa na jopo la majaji watatu, je, umemwona yeyote kutoka serikalini akikiri kuwa hilo lilikuwa kosa hivyo warejeshewe senti walizokatwa na waajiri wao?
Kiongozi wa serikali anajulikana. Hivyo basi, si sawa kumlinganisha Ruto na Zakayo kwa sababu hajatimiza mambo aliyofanya Zakayo, mwanzo kwa kutokubali kuwa ilikuwa dhambi kubwa kuwashtua Wakenya na makato ya ziada bila kuwaandaa kisaikolojia.
Pili hajashuka bado, Zakayo alishuka hasa, kwa maana ya kuacha hulka yake ya kuibia umma kupitia kwa tozo. Huku kushuka kwa Wakenya kuna maana ya kitamathali.
Yaani kubadilika na kuendesha nchi vyema ili raia wasidhanie kuwa wanaonewa. Haikutosha Rais kuvunja baraza lake la mawaziri, alirejesha nusu yake. Baadhi walibadilishiwa afisi na bado wanapumua hewa safi ya serikali.
Baada ya maandamano ya Gen – Z yameibuka mafumbo mengine hata zaidi. Shughuli za Adani nchini zimeifanya serikali kukwea mlima wa kuutetea huo ushirika kwa dhati.
Paul Nabiswa ni Mhariri, NTV