Makala

Jamaa auawa kwa kujaribu kushauri kakake asioe mke mwenye watoto sita

Na MWANGI MUIRURI October 31st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

UGOMVI kati ya kaka wawili Kaunti ya Murang’a kuhusu iwapo mmoja alipaswa kumfukuza mkewe na watoto wawili ili kuoa mwingine, mama wa watoto sita, ulisababisha kifo cha mmoja wao.

Wilfred Ndung’u, 41, dereva wa teksi, alikufa kwa sababu ya kupinga uamuzi wa kakake mdogo Peter Thuo kubadilisha mke na kujitwika mzigo mkubwa wa ndoa.

Kulingana na Naibu Kamishna wa Kaunti ya Kandara Peter Maina, kaka huyo alikuwa na biashara ya teksi katika mji wa Kenol huku mshukiwa wa mauaji akifanyya vibarua ili kujikimu.

“Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa Bw Ndung’u alikuwa amefika nyumbani baada ya kazi na alikuwa amelala kwenye sofa akiwa ameinua uso aliposhambuliwa,” akasema.

Kulingana na Bw Maina, Thuo, ambaye aliishi katika nyumba iliyo karibu, kwanza aliuliza mke wa Ndung’u alikokuwa kaka yake.

“Mke wa marehemu, Nancy Wanjiru, ambaye alikuwa nje jikoni akimpashia moto chakula mumewe, bila kushuku lolote, alimweleza Bw Thuo kwamba mumewe alikuwa ndani ya nyumba,” Maina aliambia Taifa Leo.

Katika taarifa yake kwa polisi, Bi Wanjiru anasema kuwa “shemeji yangu alikuwa na mazoea ya kumtembelea mume wangu na sikushuku kwamba ziara hii ya mwisho ingekuwa ya kusikitisha.

Aliongeza kuwa “Thuo alikuwa mlevi na alikuwa na tabia ya kutumia dawa za kulevya, alipenda kuzua ubishi na hivi majuzi, alipendekeza kubadilisha wake, mume wangu alipinga”.

Kulingana na mzee wa kijiji Stephen Mbuthia, tofauti zao kubwa ilikuwa ni hamu ya Thuo kumfukuza mkewe ambaye alikuwa na watoto wawili ili kuoa mwingine—mkubwa kuliko yeye na mama wa watoto sita.

“Suala hilo lilikuwa limeripotiwa kwa wazee na tarehe ya usuluhishi ilikuwa bado haijapangwa. Ndung’u alipinga uamuzi wa kakake mdogo akihisi haukuwa wa busara,” alisema.

Ni mzozo huu ambao unaaminika kuwa ulisababishia kaka yake hasira na akamshambulia kakake.

Wanjiru alisema kuwa “nilipomwelekeza Thuo nyumbani kwangu kukutana na kaka yake, dakika moja baadaye hivi, nilisikia sauti”.

Alisema sauti ilitoka kwa Thuo na maneno yake yalikuwa kwamba: “Unaamini wewe ndiye mwanamume pekee katika boma hili mwenye haki ya kuwa na mke huku ukipinga mimi kuwa na mke?'”.

Alisema alimwona Thuo akiondoka nyumbani akiwa na uso uliobadilika sana ambao ulimtisha.

“Nilipomtazama usoni nikashuku kwamba alikuwa amefanya jambo kubwa nyumbani kwangu…nilikimbia pale na nikaona mume wangu akiwa amelala kwenye sofa lakini damu ikitoka kwenye shimo kubwa kwenye paji la uso wake,” alisema.

Aliongeza kuwa “uwezekano ni kwamba mume wangu hakumuona kaka yake akiingia nyumbani wala kunyanyua silaha iliyosababisha kifo chake kwa sababu alikuwa amelala kwenye sofa akisubiri nimletee chakula na baadaye, maji ya kuoga ili alale”.

Wanjiru alisema alipiga kamsa “na shemeji yangu akanisaidia kupiga kelele…akisema hajali kama yeye pia angeuawa”.

Majirani walifika na mfanyabiashara mmoja wa teksi aliitwa kusaidia kumsafirisha Ndung’u hospitalini.

Maina alisema “mtu huyo alitangazwa kuwa amefariki katika Hospitali ya Kenol na mwili ukapelekwa mochari ya General Kago kuhifadhiwa”.

Maina alisema maafisa wa polisi kutoka Kituo cha Polisi cha Kabati na wa kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), walikimbia hadi eneo la tukio katika kijiji cha Gitura.

“Katika eneo la  tukio, nyundo nyeusi iliyokuwa na damu ilipatikana. Pia ilibainika kuwa marehemu alivamiwa akiwa amelala kwenye sofa iliyokuwa sebuleni kwa kuwa lilikuwa imelowa damu,” aliongeza.

Alisema Thuo alikamatwa nyumbani kwake na kufungiwa katika Kituo cha Polisi Kabati akisubiri kufunguliwa mashtaka ya mauaji.

“Ni kesi ya kusikitisha ya kufanya maamuzi kwa kukurupuka. Uamuzi huo mbaya sasa umemfanya mwanamke mwenye watoto wanne kuwa mjane huku mtuhumiwa wa mauaji akimuacha mkewe na watoto wawili,” alisema.

Imetafsiriwa na Benson Matheka