Vitu vya kufahamu katika uandishi na utahini wa insha za KCSE
UANDISHI wa insha unadhamiria kutathmini uwezo wa mtahiniwa kuwasiliana na msomaji na kuwasilisha ujumbe kimaandishi, akizingatia mada aliyopewa kikamilifu.
Mawasiliano haya yatategemea ukwasi wa lugha wa mtahiniwa. Kwa kutegemea maagizo ya swali lenyewe na umahiri wa lugha, ni lazima kutilia mkazo mtindo, mada na uwezo na mtahiniwa kufuata maagizo vilivyo.
Mtahini anapotahini kazi ya mtahiniwa, lazima aisome insha yote huku akikosoa makosa ya sarufi na hijai. Mtahini pia aangalie kwa umakini jinsi ambavyo maudhui yamejadiliwa katika kazi ya mtahiniwa.
Ukwasi wa misamiati hutahiniwa kwani hufanya insha kuwa ya kunata zaidi. Mtahini pia hutahini mtindo katika insha husika. Insha huwa na maswali manne katika KCSE. Mwanafunzi anafaa kujibu maswali mawili pekee kati ya yale manne.
Swali la kwanza huwa la lazima na huhusu insha za kiuamilifu kama vile barua rasmi, hotuba, kumbukumbu, ripoti, barua kwa mhariri, tahariri, wasifu, mahojiano, memo, tawasifu, barua ya kirafiki, n.k.
Swali la pili aghalabu huhusu kujadili masuala ibuka kwa kutoa maelezo ya kina kuyahusu.
Swali la tatu mara nyingi huhusu insha ya methali. Kisa kiwe kimoja tu, maana ya methali husika ilengwe, yaani mtahiniwa aelewe maana ya methali hiyo kikamilifu, mapambo ya lugha na ubunifu wa hali ya juu vizingatiwe.
Swali la nne kimsingi huwa ni insha ya kubuni hasa ya mdokezo. Maneno ya mdokezo yadumishishwe na kuzingatiwa katika kisa. Pawe na ubunifu wa hali ya juu huku mitindo mbalimbali ya sentensi ikitumiwa kwa ufundi na umakini.
Vitahiniwa:
(i) Kichwa cha insha
• Mtahiniwa asiweke kitone au nukta baada ya kichwa cha insha.
• Katika insha ya kiuamilifu, kichwa kitaje aina ya insha inayoshughulikiwa. Kwa mfano: HOTUBA KUHUSU NAMNA YA KUPAMBANA NA MAGONJWA CHINI
• Katika swali la tatu, mtahiniwa atumie methali aliyopewa kama kichwa cha insha. Asitumie methali mbadala au nyingine tofauti na aliyopewa.
• Katika swali la nne, mtahiniwa atoe kichwa kulingana na swali aliloulizwa. Mfano: SAFARI YA AJABU
• Aghalabu kichwa kiwe katika herufi kubwa na kipigiwe mstari mmoja tu.
• Insha zote sharti ziwe na kichwa/vichwa.
(ii) Maudhui
• Mtahiniwa aandike maudhui ya kutosha – zaidi ya manane.
• Aya iwe ya mraba kisha mstari mmoja urukwe kabla ya kuanza aya nyingine.
• Kila aya iwe na maudhui yake japo yanaweza kuchangiana.
• Maudhui yajadiliwe kwa kina.
• Uhalisia uzingatiwe katika insha ya kwanza na ya pili.
• Maudhui yajitokeze wazi hasa katika sentensi za mwanzo kwenye kila aya – sentensi tasnifu.
• Katika swali linalohitaji suluhisho, suluhisho hilo lijitokeze katika kila sentensi ya mwisho kwenye kila aya.
• Katika swali lililo na sehemu mbili (faida na hasara), pande zote ziangaziwe na msimamo kutolewa kwa kuegemea sehemu iliyo na hoja nyingi.
Mtindo mzuri ni wa kuwa na hoja tano upande mmoja na hoja tatu upande wa pili jibu likiwa na hoja nane.
(iii) Mtindo
• Mtahiniwa afahamu sura ya insha hasa za kiuamilifu.
• Azingatie urefu wa maneno 400.
• Azingatie nafsi na nyakati kulingana na aina ya insha.
• Unadhifu wa insha uzingatiwe.
• Asikatekate silabi kiholela.
• Aonyeshe nambari ya insha anayojibu kikamilifu.
• Aandike herufi vizuri bila kuzirembesha.
• Asitenganishe maneno visivyo. Mfano: ‘aliye kuja’ badala ya ‘aliyekuja’.
• Asiunganishe maneno visivyo. Mfano: ‘kwasababu’ badala ya ‘kwa sababu’.
• Vifupisho visitumike pasipofaa.
• Mtiririko na mshikamano wa mawazo uwepo.
• Insha iandikwe kwa kutumia hati nzuri.
• Matumizi ya tamathali za usemi hurutubisha insha.
• Sentensi komavu na zenye mnato zitumiwe.