Jamvi La Siasa

Raila hataki tena? Wabunge wapinga cheo cha waziri mkuu, kinara wa upinzani

Na DAVID MWERE, ERIC MATARA October 31st, 2024 Kusoma ni dakika: 3

KAMATI ya Bunge imekataa pendekezo la Rais William Ruto la kutaka kufanyia marekebisho katiba na kubuni afisi ya Kiongozi wa Upinzani.

Wabunge walisema hatua kama hiyo itadhoofisha mfumo wa serikali nchini Kenya ambayo inatumia mfumo wa urais.

Na baadhi ya wanachama wa Kamati ya Haki na Masuala ya Kisheria (JLAC), hasa wale wa ODM, pia walikataa pendekezo la kufanyia marekebisho katiba ili kuunda afisi ya Waziri Mkuu.

Walisema afisi hiyo hailingani na muundo wa utawala uliopo na ‘huenda’ itagongana na afisi ya Naibu Rais.

“Mfumo wa utawala ni wa urais. Kifungu cha 108 cha katiba kinatoa nafasi kwa viongozi wa vyama katika Bunge la Kitaifa na wanajumuisha kiongozi wa chama cha wachache ambaye kimsingi ndiye kiongozi wa upinzani bungeni,” ripoti ya JLAC inaongeza.

Wakati huo huo, mizozo ya kisiasa kati ya magavana na wawakilishi wa wadi imetatiza shughuli na kukwamisha miradi muhimu katika kaunti mbalimbali.

Migogoro hii imesababisha magavana na mawaziri wa serikali zao kutimuliwa ofisini na kusababisha ukosefu wa utulivu unaofanya serikali za kaunti kushindwa kutoa huduma.

Maspika na Viongozi walio wengi pia hawajasazwa huku wengi ambao hawakutaka kutajwa majina wakiambia Taifa Leo kwamba wanaishi kwa huruma ya madiwani.

Katika kaunti kama vile Meru Nyamira, Nakuru, Bomet na Kericho, mizozo ya mara kwa mara imesababisha shughuli za mabunge yenyewe kukwama.

Katika Kaunti ya Nyamira, Gavana Amos Nyaribo alinusurika majaribio mawili ya kutimuliwa huku akishutumiwa kwa utovu wa nidhamu, matumizi mabaya ya ofisi na ukiukaji wa sheria.

Jaribio la kwanza la kumuondoa lilikuwa Oktoba 2023 na la hivi punde zaidi lilitokea Septemba 17, 2024.

Msukosuko unaoendelea umesababisha kukatika kwa mawasiliano kati ya gavana huyo na baadhi ya madiwani. “Natoa wito kwa viongozi wote kuwa watulivu. Wacha madiwani washirikiane na gavana ili kumwezesha kufikia malengo ya utawala wake. Kuna haja ya amani huko Nyamira ili manifesto ya gavana itimizwe,” akahimiza James Ombati, mtaalamu wa eneo hilo.

Kulingana na ripoti ya hivi punde ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu, miradi ya thamani ya Sh 673.7milioni imekwama na mingine kusalia kutelekezwa kote Kaunti ya Nyamira.

Kilele cha vita kati ya bunge hilo na gavana kilikuwa Oktoba 24 wakati  madiwani walipomtimua spika Enock Okero, wakimtuhumu kwa utovu wa nidhamu miongoni mwa mashtaka mengine.

Katika Kaunti ya Nakuru, mvutano kati ya utawala wa Gavana Susan Kihika na bunge la kaunti  mwezi uliopita ulisababisha kuondolewa madarakani kwa Kiongozi wa Wengi Alex Langat, ambaye alilaumiwa kwa kutatiza jukumu la usimamizi la madiwani.

Bw Langat, mshirika wa karibu wa Gavana Kihika, alikabiliwa na msukosuko huku madiwani wote 31 wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) wakipiga kura kwa kauli moja kumwondoa madarakani.

Bw Msuri alimshutumu Bw Langat kwa kuwalinda wafisadi ndani ya Serikali ya Kaunti ya Nakuru wasiwajibike.

Kaunti ya Meru, madiwani wamemtimua Gavana Kawira Mwangaza wakitaja utovu wa nidhamu, utumizi mbaya wa afisi na upendeleo kama sababu za vitendo vyao.

Madiwani wanamkosoa Bi Mwangaza kwa kukosa kuwashirikisha katika maamuzi muhimu. Gavana huyo amekabiliwa na changamoto nyingi na alirejeshwa kwa muda na mahakama ikisubiri kusikiliza na kuamua kesi aliyopinga kutimuliwa kwake.

Katika Kaunti ya Bomet,  mawaziri watatu—Wesley Sigei (Fedha), Dkt Joseph Kirui (Utawala), na Erick Ngetich (Barabara)—walitimuliwa na madiwani mwezi uliopita lakini kwa sasa wanajadiliana kuhusu kuondoka kwao na Gavana Prof Hillary Barchok.

Gavana Dkt Erick Mutai wa Kaunti ya Kericho alikabiliwa na hali sawa ya kuondolewa ofisini na madiwani lakini akaokolewa na Seneti.

Licha ya wito wake wa maridhiano, mvutano unaendelea kati yake na kundi la madiwani.

Katika tukio lingine, Spika wa Migori Charles Likowa aligogana na madiwani  mnamo Aprili 2024, kwa madai ya kushughulikia vibaya masuala ya Bunge.

Migogoro ya mara kwa mara kati ya  madiwani  na magavana na kuhusisha  mawaziri, Maspika wa mabunge ya kaunti, na Viongozi wa Wengi, imeibua hofu miongoni mwa wataalam wa utawala.

Wengi wanahoji kuwa mamlaka ya kuondoa madarakani yaliyotwikwa madiwani yanatumiwa vibaya.

“Mamlaka ya madiwani kuwaondoa mamlakani wakuu wa kaunti  yanapaswa kuchukuliwa kama tishio ya hivi punde kwa ugatuzi, na kama hayatadhibitiwa, yatakwamisha utoaji wa huduma. Katika kaunti nyingi,  madiwani wamegeuka kuwa makundi ya wahuni, na hivyo kuweka mfano hatari,” akaonya Bw David Ngugi, mtaalamu wa masuala ya utawala.

Imetafsiriwa na Benson Matheka