Habari za Kaunti

Pigo kwa Timamy madiwani wakikataa naibu gavana mpya, hatua inayotajwa kuwa siasa za ubabe

Na KALUME KAZUNGU October 31st, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NI pigo jingine kwa Gavana wa Lamu, Issa Timamy baada ya uteuzi wa naibu wake kumrithi Bw Raphael Munyua Ndung’u, aliyefariki mwezi uliopita, kukataliwa na madiwani.

Jumatano, Bunge la Kaunti ya Lamu lilipiga kura na kuiangusha hoja ya kumpiga msasa na kumuapisha Bw James Gichu ambaye ndiye aliyekuwa ameteuliwa na Bw Timamy wiki mbili zilizopita kujaza pengo lililoachwa na marehemu Munyua.

Munyua, 46, alifariki katika Nairobi Hospital mnamo Septemba 6 mwaka huu. Alikuwa akitibiwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi akiugua.

Alizikwa kijijini kwao Umoja, tarafa ya Mpeketoni, kaunti ya Lamu Septemba 19, 2024.

Katika kikao cha Bunge la Kaunti ya Lamu kilichoandaliwa Jumatano alasiri, madiwani, chini ya uongozi wa Spika Azhar Ali Mbarak, waliafikiana kwa kauli moja kwamba wapige kura ya moja kwa moja kumuidhinisha au kumwangusha Bw Gichu bila kuwepo kwa mijadala yoyote ya hoja hiyo bungeni.

Hoja yenyewe ya pendekezo la jina la James Gichu kuteuliwa na Bw Timamy ilikuwa imewasilishwa Bungeni na Kiongozi wa Wengi, ambaye pia ni Mwakilishi wa Wadi ya Kiunga, Bw Bwana Mohamed Bwana.

Ni Diwani mmoja, Bi Mercy Wangeco kati ya madiwani wote 19 wa Lamu ambaye hakuwa bungeni wakati hoja hiyo ilipowasilishwa.

Aidha kati ya madiwani wote 18 waliokuwepo, Tisa (9) walipiga kura kuunga mkono hoja ilhali tisa (9) wengine wakiupinga. Kwa mujibu wa Katiba, matokeo hayo yaliashiria kuwa Bunge halikuweza kuipitisha hoja kulingana na kiwango cha chini kabisa cha kura kinachohitajika ambacho ni angalau zaidi ya nusu ya madiwani walioko bungeni (yaani Simple Majority in the House vote).

Hii inamaanisha hoja ilikufa au kuangushwa bungeni, hivyo uteuzi wa Bw Gichu ulikataliwa na madiwani.

Uamuzi huo wa Bunge utamlazimu Gavana Timamy kuanza tena upya mchakato mzima wa kutafuta chaguo lingine la mrithi wa naibu wake katika kipindi cha siku 14 zijazo kabla ya kuwasilisha jina hilo kwa madiwani bungeni Lamu ili kupigwa msasa na kuidhinishwa.

Hatua ya madiwani ya kumkataa Bw Gichu kuwa Naibu Gavana wa Lamu hata hivyo imepokelewa kwa hisia mseto.

Bw Ahmed Yusuf, ambaye ni mzee wa Lamu, aliwasihi wananchi kuheshimu maamuzi ya bunge, akitaja kuwa anaamini hatua yao ya kumkataa Bw Gichu ina sababu bayana na kwamba ni kwa manufaa ya umma.

“Tufahamu kwamba Bunge letu la Kaunti limepewa nguvu kikatiba kukubali au kukataa teuzi mbalimbali zinazofikishwa bungeni. Lazima tuheshimu maamuzi ya madiwani wetu wala tusisikie Vibaya. Lazima kuna sababu ya Bw Gichu kukataliwa na madiwani wetu na yote ni kwa manufaa yetu,” akasema Bw Yusuf.

Mwenyekiti wa Bodi ya Vyuma Vikuukuu nchini, Francis Mugo, ambaye ni mzawa wa Lamu, aliwafokea madiwani wa Bunge la Kaunti ya Lamu kwa kile alichokitaja kuwa ni kuendeleza siasa za ubabe badala ya kuangazia maendeleo kwa wananchi.

Bw Mugo alisema katu haoni sababu za madiwani kutupilia mbali uteuzi wa Bw Gichu kuwa Naibu Gavana wa Lamu.

“Madiwani lazima wajitokeze wazi kutueleza sababu za kwa nini walitupilia mbali uteuzi wa Bw Gichu kama naibu gavana wa Lamu. Bw Gichu amehudumu kama waziri wa Kilimo, Unyunyizaji Maji na Utoshelevu wa Chakula eneo hili tangu 2022 hadi sasa. Ana vigezo vyote vinavyompasisha yeye kuhudumu kama naibu gavana. Tumechoshwa na hizi siasa za ubabe zinazoendelezwa na madiwani wetu pale bungeni Lamu,” akasema Bw Mugo.

Naye msomi wa Lamu, Edward Mbuthia, aliwasihi madiwani kuondoa tofauti zao za kisiasa na badala yake kufanya maamuzi yanayofaa na yenye kumjenga mwananchi.

Bw Mbuthia alishangazwa na hatua ya madiwani kutupilia mbali uteuzi wa Bw Gichu kuwa Naibu wa Gavana Timamy.

“Wajua Naibu Gavana ndiye msaidizi mkuu wa Gavana mwenyewe. Ninaamini Bw Timamy alipofanya uteuzi wa Bw Gichu alikuwa ametafakari vilivyo, kuridhika na kukubali kwamba chaguo hilo ndilo linamfaa ili kusaidiana kufanikisha utendakazi wake. Inakuwaje leo madiwani wakatae. Waache siasa zisizo na mwelekeo na wampasishe huyu Gichu. Hata mimi binafsi naona anafaa,” akasema Bw Mbuthia.