Habari za Kitaifa

KINDIKI NDIYE: Kibarua cha Kithure ‘kuponya’ Mlima baada ya Gachagua kupigwa teke

Na MWANGI MUIRURI November 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NAIBU Rais mteule Profesa Kithure Kindiki huenda akawa na wakati mgumu kisiasa katika muda wa miaka mitatu ijayo baada ya kuchukua wadhifa wa mtangulizi wake Rigathi Gachagua.

Prof Kindiki, ambaye amepanda cheo upesi katika muda wa miaka miwili kutoka wadhifa wake wa awali wa Waziri wa Masuala ya Ndani, atakabiliwa na dhoruba inayoendelea katika Mlima Kenya.

Huku Mlima Kenya ukikabiliwa na hali ya wasiwasi, kazi ngumu zaidi ya Prof Kindiki itakuwa kushawishi eneo hilo kumuunga mkono Rais William Ruto ilivyokuwa katika uchaguzi wa 2022.

Prof Kindiki pia anachukua nafasi ya Bw Gachagua kama naibu kiongozi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) alivyosema Katibu Mkuu wa chama hicho Bw Omar Hassan mnamo Jumatano.

Atatarajiwa kuongoza uchaguzi wa mashinami wa chama haswa katika Mlima Kenya ambao ulisimamishwa kufuatia siasa za sumu zinazoshuhudiwa katika eneo hilo.

Jukumu la kuunganisha tena eneo lilitatizwa na kuondolewa kwa Bw Gachagua.

Hii ni kazi ambayo Seneta wa Nyandarua Bw John Methu anataja kama ‘ni ngumu kupindukia’.

“Mlima umesumbuliwa na uko katika hali mbaya kwa sasa na jinsi Kindiki na mrengo wake wananuia kutuliza ili kuepuka kulipuka sio kazi ambayo ningependa mabegani mwangu,” Bw Methu aliambia Taifa Leo.

Mbunge wa Githunguri Bi Gathoni wa Muchomba pia alisema “ndugu yangu anayeheshimika Kindiki atahitaji neema ya Mungu ili kupambana na dhana kwamba alitumiwa kugawanya Mlima Kenya na kumsaliti Gachagua asulubiwe ili apate manufaa ya binafsi”.

“Tuko katika hali ya kusubiri. Mtu yeyote asimdanganye Bw Kindiki kwamba itakuwa rahisi,” alisema seneta wa Murang’a, Joe Nyutu.

Imetafsiriwa na BENSON MATHEKA