Jina ‘Abra K’ litashika kama la ‘Riggy G’?
RAIS William Ruto ameonekana kuendeleza mtindo wa naibu wake kujulikana kwa jina la utani kwa kumpachika naibu wake mpya Kithure Kindiki jina “Abra K”.
Akihutubu Ijumaa katika uwanja wa KICC, Nairobi baada ya Profesa Kindiki kulishwa kiapo, Dkt Ruto alimtaka Profesa Kindiki kumsaidia kutekeleza ajenda za Serikali ya Kenya Kwanza kwa manufaa ya Wakenya.
“Nakukaribisha ndugu yangu, Abraham Kithure Kindiki, na nikubalie nikuita Abra K, tuwahudumie wananchi na taifa la Kenya. Kwa sababu amejaaliwa kipawa kwa kuzungumza kwa ufasaha, nisaidie kuangazia mipango na miradi ambayo serikali hii imefaulu kutekeleza na inaendela kutekeleza,” Rais akasema.
“Ni matumaini yangu utatenda yale ambayo nimekosa kwa miaka miwili iliyopita, kwa sauti yenye ufasaha mkubwa,”Dkt Ruto akaeleza.
Huku akionekana kumpiga vijembe aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Rais Ruto, alimtaka Profesa Kindiki kuwahudumia Wakenya wote “kwa haki, usawa, bila ubaguzi wala woga.”
“Nakutaka ewe “Abra K”, kutekeleza majukumu yako bila kuongozwa na ubaguzi kwa misingi ya familia, kabila au eneo. Uwatumikie Wakenya wote kwa asawa kwa sababu wewe ni Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya,” akaeleza.
Bw Gachagua ambaye aliondolewa afisini mnamo Oktoba 17, 2024 amekuwa akijulikana kwa jina la utani la Riggy G.
Jina hilo alipewa miezi michache baada ya kuingia mamlakani mnamo Oktoba 17, 2022 na mwanafunzi wa chuo kikuu kwa jina Ivy Chelimo.
Baadaye Bw Gachagua alimwakilika mwana dada huyo afisini mwaka Jumba la Harambee Annex B na kuahidi kumpa ajira afisini humo.