Fahamu jinsi ya kusajili ndoa za kitamaduni
BAADHI ya wasomaji wameomba ufafanuzi zaidi kuhusu ndoa za kitamaduni na zinavyosajiliwa. Baadhi ya wasomaji wanataka kujua iwapo ndoa za kitamaduni zilizodumu za mababu walio hai zinapaswa pia kusajiliwa.
Nitaanza kwa kueleza kuwa ndoa ya kitamaduni ni ile inayofanyika kwa kufuata mila na desturi za jamii ya wachumba wawili- mwanamume na mwanamke-au inayofanyika kwa kufuata desturi za jamii ya mmoja wao.
Usajili wa ndoa za kitamaduni nchini Kenya unasimamiwa na Kanuni za Ndoa (Ndoa ya Kitamaduni) 2017, chini ya Sheria ya Ndoa. Kanuni hizi zilitekelezwa na Notisi ya Gazeti Rasmi la Serikali Nambari 5345 iliyotolewa Juni 9 2017.
Kulingana na notisi hiyo, ndoa zote za kitamaduni zilipaswa kuanza kusajiliwa Agosti 1 2017. Ilifafanua zaidi kuwa ndoa za kitamaduni zilizokuwemo kabla ya Agosti 1 2017 wahusika wanatakiwa tu kusajili ndoa na kupewa cheti cha ndoa.
Usajili wa ndoa ya kitamaduni unahusisha wahusika wawili kufika mbele ya msajili,wa ndoa ambaye anawahoji ili kubaini uhalali wa ndoa hiyo na ikiwa wahusika wote wawili ni watu wazima waliokubali kuoana kwa hiari yao.
Maombi ya usajili hufanywa kwa kujaza fomu inyoambatana na barua ya uthibitisho kutoka kwa chifu wa eneo ambalo sherehe ya ndoa ya kitamaduni ilifanyika.
Kulingana na kanuni za ndoa za kitamaduni, fomu hiyo inajumuisha ithibati kwamba kati ya wanandoa hao hakuna aliye na umri mdogo, kwamba walikubali ndoa hiyo kwa hiari, kwamba hakuna hata mmoja wao aliyekuwa katika ndoa ya kijamii, ya Kikristo, ya Kihindu na ya Kiislamu na kwamba hakuna kizuizi kinachozuia ndoa hiyo.
Wanandoa hulipa ada ya usajili wa ndoa na kupatiwa risiti rasmi. Kabla ya kusajili ndoa ya kitamaduni, msajili anaweza kufanya uchunguzi zaidi inapobidi. Ni muhimu kufahamu kuwa wanandoa wote wawili ni lazima wafike kila mmoja binafsi mbele ya Msajili wa ndoa na hakuna kuwakilishwa.
Kulingana na notisi niliyotaja hapa juu, wanaofunga ndoa za kitamaduni baada ya tarehe ya kuanza kutumika kwa kanuni za kusimamia ndoa za kitamaduni, wanatakiwa kumjulisha msajili kuhusu hali yao ya kuwa mume na mke ndani ya miezi mitatu (3) baada ya kukamilika kwa taratibu za kitamaduni za jamii wanaozotumia kufunga ndoa yao.
Taarifa hiyo inatolewa katika fomu wakieleza jamii ambayo walitumia desturi zake kufunga ndoa, tarehe ya kufunga ndoa, mahali ambapo ndoa ya kitamaduni ilifungwa, taarifa za wazazi wa wanandoa pamoja na kazi yao.
Vile vile, pande zote zinapaswa kufika mbele ya msajili binafsi pamoja na mashahidi wao. Aidha, wanapaswa kuambatisha picha za saizi ya pasipoti na nakala za vitambulisho vya kitaifa vya mashahidi.