Hivi ndivyo nitafanya ili msiwe mayatima, Gachagua aambia Mlima
ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua, amewaambia wafuasi wake hasa katika Mlima Kenya wasiwe na hofu kuhusu kuondolewa kwake mamlakani, na akaahidi kuwapa mwelekeo mpya wa kisiasa.
Bw Gachagua alizungumza Jumamosi huku washirika wake wakiongozwa na Seneta wa Kirinyaga Kamau Murango wakimtaka kuunda chama cha kisiasa ambacho atatumia kutafuta kiti cha kitaifa katika uchaguzi wa 2027 na kujadiliana kupata mgao wa rasilimali za kitaifa.
Akizungumza katika Kanisa la Kianglikana la Kiamwathi kaunti ya Kirinyaga wakati wa ibada ya mazishi ya Anna Wanjiru, nyanyake Diwani David Mathenge wa wadi ya Baragwi, Bw Gachagua alisema kuwa kulikuwa na wasiwasi na mkanganyiko katika eneo hilo lenye wapiga kura wengi baada ya kung’olewa haraka kutoka katika kiti chake na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki.
Alilalamika kwamba alitimuliwa ofisini haraka sana na akaapa kupigania maisha yake ya kisiasa.
“Siachi siasa, azma yangu ya kisiasa haiwezi kuzimwa na nawaomba wafuasi wangu ambao wanaona kana kwamba wameachwa bila kiongozi wawe na subira, hivi karibuni nitawaonyesha njia ya kisiasa ya kufuata,” alisema.
Alisema anaelewa kuwa wakazi wa Mlima Kenya hawakufurahishwa na kilichompata na wanahisi kutelekezwa.
“Viongozi wa kidini, wakazi na wataalamu wamekuwa wakinipigia simu wakisema ukanda huu umeachwa bila msemaji, wanataka nitangaze msimamo wangu wa kisiasa. Nitawapa mwelekeo wa wazi wakati ufaao,’ alisema.
Akiwa ameandamana na mkewe, Mchungaji Dorcas, Naibu Rais huyo wa zamani aliwahakikishia wakazi kwamba hatawaacha.
‘Sina ujanja sana lakini mimi si mjinga, kama kiongozi wenu nitawaonyesha njia ya kusonga mbele. Ninataka watu wetu wasiogope hata kidogo. Mungu ni mwaminifu na hawezi kushindwa,’ alisema.
Bw Gachagua alitetea rekodi yake ya maendeleo akisema kamwe hakuwaangusha Wakenya.
‘Nilipewa kazi ya kurekebisha sekta ya kahawa na Rais William Ruto. Nilifanya kazi yangu ipasavyo na Mswada wa Kahawa unasubiri kuwasilishwa katika Bunge la Kitaifa,’ akasema.
Aliwaambia wabunge waliomuondoa mamlakani kupitisha Mswada huo ili Wakenya wanufaike.
‘Ninawaomba Wabunge kwamba kasi ile ile waliyoonyesha Bungeni ya kuniondoa ofisini, waitumie kupitisha Mswada wa Kahawa,’ alisema.
Aliwataka wakazi hao kutokubali kugawanywa na watu kutoka nje ya Mlima Kenya.
‘Kama hatutaungana, tutamalizwa kisiasa. Tuliposhindwa kuungana, niliondolewa madarakani na hili ni jambo zito sana,’ alisema.
Washirika wa Gachagua walisema eneo la Mlima Kenya halina chama cha kisiasa na ndiyo maana lilikuwa likipigwa vita na kunyimwa fursa ya kuwa katika uongozi wa kitaifa.
‘Sasa tumeamka kufuatia masaibu aliyopitia kiongozi wetu Gachagua, tunapaswa kuwa na chombo cha kisiasa ili tusichukuliwe kama wageni. Mali ya kukopa si nzuri hata kidogo,’ alisema Bw Murango.
Seneta huyo alimhakikishia Bw Gachagua kwamba viongozi wa eneo hilo watasimama naye.
‘Ukitupigia simu tutapatikana na kuunga mkono azma yako ya kisiasa, hatutakubali woga kutoka kwa maadui wa kisiasa wa Gachagua,’ alisema Bw Murango.
Seneta huyo alisimulia jinsi alivyosimama kidete katika Bunge la Seneti na kukataa kumsaliti Bw Gachagua ambaye alishikilia kuwa bado alikuwa msemaji wa eneo hilo.
Naye Mwakilishi wa Wanawake wa Kirinyaga Njeri Maina alisema eneo la Mlima Kenya litakuwa salama kisiasa iwapo tu litakuwa na chama.
Imetafsiriwa na Benson Matheka