Jinsi ya kuzidisha mapato kupitia ufugaji wa kuku kiteknolojia
SIKU za hivi karibuni, vijana wengi wanatafuta njia mbadala za kujipatia kipato na kujiimarisha hasaa wanapokosa ajira.
Zabron Muthike, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya fedha, aliamua kuwekeza katika ufugaji kuku kwa kukumbatia teknolojia ili kuzidisha mapato.
Zabron amekumbatia teknolojia ambayo inamuwezesha kuangua vifaranga wengi kwa wakati mmoja ukilinganisha na mbinu za kawaida.
“Mimi hutumia kiangulio chenye uwezo wa kuzalisha vifaranga elfu tatu kwa muda wa wiki tatu tu,” anaeleza.
“Ninashauri wakulima wengine waondoke katika mitindo ya kiasili katika ufugaji ndege ili wazidishe mapato yao.”
Kulingana na Zabron anatueleza ufugaji wa kuku unaweza kumvunia mfugaji mapato makubwa endapo atafuatilia utaratibu ufaao.
“Mimi nina mashine za kuangua vifaranga na mabanda yenye mazingira mazuri ya joto kuwalea vifaranga baada ya kuanguliwa,” anaambia Akilimali.
Katika kipindi cha miezi miwili ya kwanza, vifaranga hulishwa chakula cha kuku wachanga kinachojulikana kama chick mash kabla ya kukua na kutosha kula lishe nyingine iitwayo growers mash.
Zabron hulea kuku ambao wanataga mfululizo kwa mwaka mmoja na nusu.
Lakini anachosisitiza zaidi zabron ni umuhimu wa kufuata ratiba ya chanjo na kurekodi taarifa za kila siku shambani.
Kulingana naye, hii ndiyo siri ya kuepuka hasara na kudhibiti magonjwa na wadudu wanaoweza kuathiri afya ya kuku.
Kwa ushirikiano na wakulima wenzake, Zabron ameunda chama cha ushirika ili kukuza uwezo wa kusambaza vifaranga zaidi ya elfu tatu.
Hii huwasaidia kukidhi mahitaji ya soko na kuhakikisha wana kipato cha kudumu.
Licha ya mafanikio hayo, Zabron anakiri kuwa bado kuna fursa nyingi kwenye soko la kuku ambazo hawajazichangamkia kikamilifu.
Katika kuboresha gharama, wanatumia mbinu za kulisha kuku wao kwa vyakula vya kiasili – mbinu ambazo hupunguza gharama za chakula kwa kiasi kikubwa.
“Ninatoa wito kwa vijana na wakulima wote nchini kuikumbatia teknolojia ili kufikia mafanikio ya kweli katika kilimo,” anashauri.
Kwake Zabron, ufugaji wa kuku sio tu njia ya kujichumia riziki, bali pia ni mpango wa kujijenga na kutimiza matamanio ya nafsi yake.