Polisi waonywa dhidi ya kufungia watoto kwa seli za watu wazima
Na Vitalis Kimutai
POLISI katika Kaunti ya Bomet wameshutumiwa vikali kutokana na hatua ambapo waliwaweka pamoja watoto na watu wazima na kuwafungia katika seli moja katika vituo vya polisi.
Hakimu Mkuu Mkazi wa eneo hilo, Kipkirui Kibelion alionekana kukasirishwa na mwenendo huo na kutoa amri kwamba, maafisa wa polisi wanapaswa kukomesha hatua kama hiyo, huku akiwataka ahakikishe watoto wanazuiliwa katika makazi ya watoto.
“Kumekuwa na mwenendo hatari, na mbaya, ambapo watoto hufungiwa katika seli mwishoni mwa juma na kuwasilishwa kortini Jumatatu. Nini kinaendelea hapa?”, Bw Kibelion akamuuliza mwendesha mashtaka wa umma, Bw Fredrick Wawire.
Bw Wawire aliiambia mahakama hiyo kwamba, hakuwa na habari kwamba watoto wamekuwa wakifungiwa ndani ya seli za polisi kinyume cha amri ya hakimu huyo. Hata hivyo, aliahidi kuwasiliana na Afisa Msimamizi wa Kituo cha Polisi Daniel Nyagako.?Hakimu huyo alisema polisi wanapaswa kuwalinda watoto lakini inaonekana maafisa katika kaunti ya Bomet wamekuwa wakikiuka agizo hilo.
“Je, polisi huwakamata watoto baada ya kufeli kuwashika wazazi wao haswa katika kesi zinazohusiana na utengenezaji na uuzaji wa pombe haramu” Mbona watoto wadogo hufungiwa katika seli za polisi kuanzia Jumamosi hadi Jumatatu?” akauliza Bw Kibelion.
Hakimu huyo aliibua maswali hayo baada ya zaidi ya watoto saba wanaokabiliwa na mashtaka mbalimbali kufikishwa mbele yake Jumatatu alasiri. Baadhi yao walikuwa wakikabiliwa na kesi za kuvunja nyumba na kuiba huku wengine wakikabiliwa na mashtaka ya kupatikana na pombe haramu.
“Amri yangu ni wazi kwamba watoto wanafaa kufungiwa katika makao ya watoto wala sio katika seli za polisi pamoja na watu wazima. Lakini inasikitisha kuwa maagizo yangu hayajazingatiwa. Naona kuna hila kubwa katika kesi hizi,” akasema Bw Kibelion.