Hoteli ya DusitD2 hatimaye yafunguliwa tena kwa umma
Na BENSON MATHEKA
HOTELI ya DusitD2 iliyoko 14 Riverside Drive, Nairobi ilifunguliwa Jumanne kwa umma wiki moja baada ya magaidi wa Al Shabab kuishambulia na kuua watu 21.
Polisi waliruhusu walioacha magari yao kuingia katika hoteli hiyo na majengo yaliyo karibu kuyachukua. Wamiliki wa afisi na biashara zilizokuwa kwenye jengo hilo pia waliruhusiwa kuingia ndani kwa mara kwanza tangu shambulizi hilo la Jumanne wiki iliyopita.
Msemaji wa polisi, Charles Owino alisema jengo la hoteli litafunguliwa kwa wapangaji na wageni waliokuwemo wakati magaidi wanne waliokuwa na bunduki walipotekeleza shambulizi hilo.
Polisi walisema watu zaidi ya 700 waliokolewa na maafisa wa usalama katika operesheni iliyochukua zaidi ya saa 15.
Kulingana na Bw Owino, wapangaji sasa wanaweza kuingia katika ofisi na biashara zao baada ya polisi kuhakikisha eneo hilo ni salama.
Polisi walizuia umma katika eneo hilo ili kuondoa vilipuzi ambavyo vilikuwa vimeachwa na magaidi ambao waliuawa Jumanne usiku.
Mabomu kadhaa yalipatikana na kupelekwa kuharibiwa. Gaidi mmoja aliyetambuliwa kama Mahir Khalid alijilipua nje ya mkahawa wa Secret Garden kabla ya wenzake kuvamia na kufyatulia watu risasi.
Polisi wanaendelea kuchunguza jinsi shambulizi hilo lilipangwa, waliolifadhili na waliosaidia magaidi hao kulitekekeza. Kufikia sasa, washukiwa 10 wamefikishwa kortini kuhusiana na shambulizi hilo. Polisi walipatiwa kibali cha kuwazuilia kwa siku 30 zaidi ili kukamilisha uchunguzi.
Waliopoteza wapendwa wao kwenye tukio hilo waliendelea kuomboleza. Leo, jamaa na marafiki wa Japhet Ndunguja Nuru afisa wa kikosi cha GSU aliyeuawa kwenye shambulizi hilo wataandaa harambee ya kusaidia katika mazishi yatakayofanyika kaunti ya Taita Taveta.
Harambee hiyo itafanyika katika kanisa la All Saints Cathedral jijini Nairobi.
Jana, jamaa, marafiki na wafanyakazi wa kampuni ya Cellulant waliandaa ibada ya kuwakumbuka wafanyakazi sita wa kampuni hiyo waliouawa na magaidi hao.