Jamvi La Siasa

Gachagua aanza kufunikwa wandani wakipanga maisha bila yeye

Na CECIL ODONGO November 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

HATA kabla ya kuku kumeza punje, aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ameanza kudondoshwa polepole huku baadhi ya viongozi waliokuwa wakimuunga mkono wakionekana kuanza maisha mapya ya kisiasa bila yeye.

Matumaini ya Bw Gachagua kusalia kwenye wadhifa wake yalizikwa mnamo Alhamisi wiki jana, baada ya jopo la majaji watatu kuondoa amri iliyokuwa imezuia kuapishwa kwa Prof Kithure Kindiki kama naibu rais.

Hatua hiyo ilipisha kuapishwa kwa Prof Kindiki kama naibu wa rais huku Bw Gachagua akibaki kuendelea na kesi mahakamani wakati ambapo mrithi wake naye akiendelea kuchapa kazi.

Wikendi, mwandani wa Bw Gachagua ambaye ni Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga alisema naibu wa rais aliyefurushwa amekubali hatima yake ya kubanduliwa na mabunge ya kitaifa na seneti.

Hii ni baada ya baadhi ya wanasiasa kutoka Mlima Kenya kumpigia upatu awe mrithi wa Bw Gachagua katika siasa za eneo hilo.

Bw Kahiga alikuwa mtetezi mkubwa wa aliyekuwa naibu wa rais huku akikashifu sana Rais Ruto kwa kumhangaisha naibu wake kisiasa.

“Aliyekuwa naibu rais amekubali mustakabali wake wa kisiasa. Tunamwomba Rais ahakikishe kuwa Kaunti ya Nyeri inabakia kati ya maeneo ambayo anatekeleza miradi ya maendeleo,” akasema Bw Kahiga akihutubu katika sherehe ya kufuzu kwake kwa shahada ya uzamifu.

Gavana huyo alimkumbusha Rais Ruto kuwa wakazi wa Nyeri walimpigia kura hivyo basi juhudi bado zinastahili kuelekezwa katika kuinua kaunti hiyo kiuchumi kama tu maeneo mengine ya nchi.

Gavana wa Tharaka-Nithi Muthomi Njuki alisema Bw Kahiga ana sifa za kuwa kiongozi wa kitaifa zaidi ya kuwa gavana wa Nyeri pekee, kauli ambayo imefasiriwa kuwashinikiza wakazi wa Kaunti ya Nyeri wazoee maisha bila kigogo wao Bw Gachagua.

“Bw Mutahi, Kenya inakuhitaji. Umehudumia wakazi wa Nyeri vizuri lakini hufai kudhibitiwa na kuendelea kuonyesha uongozi kwenye kaunti hii,” akasema Bw Njuki ambaye anatoka kaunti anakotoka Prof Kindiki.

“Watu wa hapa Nyeri ni majirani zetu wazuri. Tusiruhusu kile ambacho kimefanyika kitutenganishe kwa sababu sote tunakumbwa na tatizo moja na hatufai kuruhusu siasa itugawanye,” akaongeza.

Mwakilishi wa Kike wa Kirinyaga Anne Njeri ambaye pia alikuwa jemedari wa Bw Gachagua, amemwambia aanze ushirikiano na viongozi wengine akiwemo Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka ili kuleta mwamko mpya wa kisiasa nchini.

Kauli hii inaonekana kulenga siasa za baadaye kwa kuwa iwapo kesi iliyo mahakamani itaishia kuhalalisha kuondolewa kwa Bw Gachagua basi huenda akazimwa kushikilia cheo chochote cha umma.

Viongozi kutoka ukanda wa Mlima Kenya wamedai kuwa Bw Gachagua alifurushwa serikalini kwa urahisi kwa sababu aliingia kwenye mkataba wa kisiasa na Rais Ruto bila kuwa na chama cha kisiasa.

Seneta wa Kirinyaga James Murango alisema kuwa lazima eneo hilo liwe na chama chake cha kisiasa ili lisichukuliwe kama mgeni kwenye vyama vingine.

“Mali ambayo imekopeshwa si nzuri ndiposa kutokana na masaibu ambayo yalimpata Bw Gachagua, lazima tuanze kuwa na chama chetu cha kisiasa,” akasema Bw Murango.

Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Prof Macharia Munene mamlaka ndiyo yalikuwa yanamfanya Bw Gachagua awe na umaarufu kwa kuwa sasa hayapo, lazima utashuka.

“Kusahaulika atasahaulika pole pole. Unaibu Rais ndio ulikuwa unampa umaarufu japo bado ana jina na bado atakuwa na ushawishi hapa na pale kwa kutegemea jinsi ambavyo atacheza siasa zake,” akasema Prof Munene.

Mchanganuzi huyo aliongeza kuwa matokeo ya kesi kortini pia yatakuwa na athari kwenye siasa za Bw Gachagua na akijipanga vizuri, bado atakuwa na Mlima Kenya.

“Hata akifungiwa, miaka 10 ni michache sana kwa mwanasiasa na akimchagua mtu wa kuunga ambaye atafanya vizuri uchaguzini, basi siasa zake hazitaisha,” akaongeza Prof Munene.

Viongozi wengine wa kisiasa wanaopigiwa upatu kutwaa nafasi ya Bw Gachagua kama Msemaji wa Mlima Kenya wanajumuisha Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru, Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua na Gavana wa Murang’a Irungu Kang’ata.