• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Pasta atimua polo kumtamani bintiye kanisani

Pasta atimua polo kumtamani bintiye kanisani

NA JOHN MUSYOKI

MACHAKOS MJINI

KISANGA kilizuka katika kanisa moja hapa jamaa alipofurushwa kwa madai ya kuharibu binti ya pasta. Inasemekana jamaa alikuwa mgeni katika kanisa hilo aliposimama kusalimia waumini na kudai nia yake ilikuwa ni kuoa binti ya pasta.

Matamshi yake yalimkera mtumishi wa Mungu na akamnyang’anya kipaza sauti na kumwamuru aondoke kabla ya kumchukulia hatua. “Kijana wewe, toka nje mara moja kabla sijachemka kwa hasira. Wewe ni nani na sijawahi kukuona hapa wala hujaja kwangu kujitambulisha?” pasta alimfokea.

Jamaa alijaribu kujitetea lakini mtumishi wa Mungu alimpuuza. “Kwanza wewe sio muumini wa kanisa hili na hauna nafasi ya kudai utaoa binti yangu mbele ya waumini bila ruhusa kutoka kwangu, kwenda kabisa!” Pasta alizidi kuchemka.

Hata hivyo, jamaa alijkakamua kujitetea lakini juhudi zake ziliambulia patupu. “Pasta kuwa mpole. Nishapendana na binti yako kwa dhati na hata usiku silali nikimfikiria. Binti yako sasa amekomaa na ana haki ya kuolewa. Kwa nini umemfunga nyumbani kama kuku, mpe uhuru wake aolewe,” jamaa alimwambia pasta

Inasemekana pasta alimrukia jamaa akitaka kumcharaza lakini akazuiliwa na waumini. “Huyu kijana anataka kumharibu binti yangu. Sitakubali hilo kutendeka. Hana hata heshima kuja hapa kanisani kutangaza anataka kumuoa binti yangu. Binti yangu sio kahaba na sitaruhusu mwanamume aliyepotoka kumharibu,” pasta alisema.

Jamaa kuona hivyo aliamua kuondoka kanisani na kwenda zake. Hata hivyo haikujulikana ikiwa alikuwa akimchumbia binti ya pasta huyo ambaye hakuwa kanisani wakati wa kisanga hicho.

Kwa mujibu wa mdokezi, pasta alikuwa mkali sana na hakurusu mabinti zake kutoka nje ya boma bila ruhusa.

You can share this post!

Machifu wakosa afisi, wachapa kazi chini ya miti

TAHARIRI: Tusilenge Waislamu katika vita dhidi ya ugaidi

adminleo