• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 AM
WASONGA: Walinzi wapewe bunduki lakini iwe kwa masharti

WASONGA: Walinzi wapewe bunduki lakini iwe kwa masharti

Na CHARLES WASONGA

NI jambo la busara kwa serikali kubadili mikakati yake ya kukabiliana na utovu wa usalama nchini, hususan, mashambulio ya kigaidi.

Hii ni kwa sababu bila kuwepo kwa usalama serikali haitaweza kutimiza malengo yake makuu ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi..

Hii ndio maana naunga mkono wazo la kuwapa walinzi wa kibinafsi, almaarufu askari gongo, bunduki kuanzia mwezi wa Julai mwaka huu.

Hii ni kwa sababu wakati wowote tukio la utovu wa usalama linapotokea, kama vile shambulio la kigaidi katika hoteli ya DusitD2 jijini Nairobi wiki iliyopita, walinzi ndio huwa wa kwanza kulengwa au kukabiliana na wahusika.

Lakini mpango huo uliotangazwa wiki jana na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kudhabiti Kampuni za Kibinafsi za Ulinzi (PSRA), Bw Fazul Mohamed unafaa kutekelezwa kwa makini kabisa ili kuzuia visa ambapo bunduki hizo zinaweza kutumiwa visivyo.

Kwanza, serikali na kampuni husika zinapasa kutenga pesa za kutosha za kuhakikisha kuwa takriban walinzi 500,000 ambao wameajiriwa na zaidi ya kampuni 1,000 zilizosajiliwa wamepewa mafunzo upya kuhusu matumizi ya silaha hizo.

Na sio mafunzo tu, kampuni husika pamoja na mamalaka ya PSRA zinapasa kuhakikisha kuwa ni askari wenye maadili mema pekee wanaopatiwa mafunzo hayo ya kutumia bunduki.

Nasema hivi kwa sababu kumekuwepo na visa ambapo polisi waliopewa mafunzo ya hali ya juu wametumia silaha zao kuwahangaisha wananchi wasio na hatia au kuzikodisha kwa wahalifu. Hii ni kwa sababu maafisa kama hawa huwa wamepotoka kimaadili.

Pili, sheria inapasa kubuniwa itakayoongoza matumizi ya bunduki katika sekta ya ulinzi wa kibinafsi. Chini ya mwavuli wa sheria hiyo, mamlaka huru ya kusimamia matumizi ya bunduki na silaha zingine hatari katika sekta ya kibinfisi inafaa kubuniwa na kupewa ufadhili wa kutosha.

Ni mamlaka kama hii ambayo itatwikwa jukumu la kushirikisha mafunzo kwa askari na kuwapiga msasa wale ambao wanapasa kupewa bunduki. Isitoshe, ni mamlaka kama hii ambayo itahifadhi habari na maelezo kuhusu bunduki zote zinazotumika na askari wa kampuni mbalimbali za ulinzi.

Kupitia njia hii, itakuwa rahisi kwa serikali kutambua askari ambao watatumia silaha zao kuendeleza uhalifu, kama vile kuzikodisha kwa wezi na wakora wengine.

Ni mamlaka kama hii ambayo vile vile itaweka viwango vya kuhitimu kwa askari ambao watapewa mafunzo ya matumizi ya bunduki.

Kwa hivyo, kamati ya bunge kuhusu usalama wa ndani inapasa kushirikiana sako kwa bako na mamlaka ya PSRA inayosimamiwa ili kuunda mswada kuhusu mabadiliko katika sekta ya ulinzi wa kibinafsi.

Mswada huo unapasa kuandaliwa mapema ili uweze kuwasilishwa bungeni mwezi ujao Bunge litakaporejelea vikao vyake baada ya likizo ndefu.

Hii ndio njia ya kipekee ya kuhakikisha kuwa mpango huu unachangia kuimarishwa kwa usalama nchini hasa nyakati hizi ambapo mashambulio ya kigaidi yameanza kutokea tena.

You can share this post!

TAHARIRI: Tusilenge Waislamu katika vita dhidi ya ugaidi

NGILA: Sheria ya utambulisho wa DNA itasaidia kuzima uhalifu

adminleo