Habari za Kitaifa

Mateso, kilio, wafanyakazi wa kaunti wakicheleweshewa mishahara kwa hadi miezi minne

Na WAANDISHI WETU November 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAFANYAKAZI wa serikali za kaunti kote nchini wanakabiliwa  na wakati mgumu kufuatia kucheleweshwa kwa mishahara kwa miezi kadhaa.

Chanzo kikuu cha masaibu yao ni uhaba wa pesa uliosababishwa na kucheleweshwa kwa mgao wa kila mwezi kwa kaunti kutoka Hazina ya Kitaifa.

Kufadhaika sasa kunaongezeka huku wafanyikazi hao wakihisi kupuuzwa—hasa baada ya wafanyikazi wa serikali ya kitaifa kupokea nyongeza ya mishahara huku wafanyikazi wa kaunti wakikosa kuzingatiwa.

Baadhi ya kaunti kama Kakamega na Kisumu zinalazimika kukopa pesa kutoka kwa taasisi za kifedha ili kulipa mishahara.

Katika Kaunti ya Bungoma, hali ni mbaya, huku wafanyikazi wakipokea mishahara wao mara ya mwisho Julai pekee. Ucheleweshaji huo umezua shida kubwa ya kifedha kwa wafanyikazi.

“Mimi ni afisa aliyevunjika moyo sana jioni hii. Nimetembelea hospitali tatu tofauti kutafuta matibabu, lakini bila mafanikio. Mbaya zaidi, sina pesa za kulipia matibabu yangu kwa sababu ya kutolipwa mshahara wangu, na hakuna habari kuhusu ni lini, au ikiwa, tutalipwa. Ni Mungu pekee anayeweza kuingilia kati ili kutuokoa kutokana na hali hii isiyovumilika—hakuna chakula, hakuna nauli, hakuna matibabu, hakuna mshahara,” akasema afisa mmoja kutoka kaunti ya Bungoma.

Kaunti za  Kusini mwa Bonde la Ufa, zikiwemo Nakuru, Laikipia, Narok, Nyandarua, na Kericho, zimegeukia mikopo ya benki ili kulipa mishahara baada ya kukosa pesa kutokana na kucheleweshwa kwa mapato.

Huko Laikipia, watumishi wa umma bado hawajapokea mishahara yao ya Septemba. Daktari kutoka Hospitali ya Nyahururu alisema kuwa, “baadhi yetu hatujalipwa kwa miezi 3 hadi 6. Wazazi wanakidhi vipi mahitaji ya watoto bila mshahara?”

Mjini Nakuru, barua iliyoandikwa Oktoba 28 kutoka kwa Katibu wa Kaunti Dkt Samwel Mwaura ilithibitisha kucheleweshwa kwa mishahara, ikitaja masuala ya kuunganisha Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii katika mfumo wa malipo.

“Tuliambiwa ucheleweshaji huo ulitokana na masuala ya makato ya SHA. Tunasubiri tu,” alisema.

Katika eneo la Pwani, Mombasa ndiyo kaunti pekee ambayo imetimiza wajibu wake wa kulipa mshahara kwa wakati. Kaunti zingine, kama vile Tana River, wafanyikazi wanasubiri mishahara, na zaidi ya wafanyikazi 2,000 bado hawajalipwa.

Huko Taita Taveta na Lamu, wahudumu wa afya na wafanyikazi wengine wa kaunti pia  hawajapata mishahara kutokana na utekelezaji wa makato ya SHIF.

“Bado hatujapokea mishahara yetu ya Oktoba na kila tunapouliza, tunaambiwa tuwe wavumilivu wakati wanaendelea na utekelezaji wa makato ya SHIF,” alisema daktari ambaye aliomba tubane jina lake kwa vile hana mamlaka ya kuzungumza na waandishi wa habari.

Imetafsiriwa na BENSON MATHEKA