Jamvi La Siasa

Wazee Mlima Kenya wawasihi Wakenya wasimtupe Gachagua

Na MARY WANGARI  November 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAZEE wa jamii za kutoka eneo la Mlima Kenya wamewasihi Wakenya kwa jumla wamsaidie aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua anapoanza maisha yake mapya baada ya kutimuliwa mamlakani.

Huku wakiwarai Wakenya wasimwache na upweke Bw Gachagua, wazee hao wa jamii ya Gikuyu, Embu, Meru na Akamba (GEMA), walikosoa jinsi alivyotimuliwa afisini.

Kupitia Muungano wa Kijamii wa GEMA (GCA), viongozi hao, walisema japo Bw Gachagua alikuwa na udhaifu wake, hakustahili aliyotendewa na viongozi wenzake na taifa kwa jumla.

“Kazi ya marais, manaibu rais, magavana na viongozi wengine ni ya muda. Inahusu huduma unayopatia taifa lakini taifa halipaswi kukurusha nje kama takataka. Badala yake, wanapaswa kukuchukulia kama mmoja wao, kaka au dada yao,” alisema Mwenyekiti wa GEMA, Bw Lawi Imathiu.

Akihutubia vyombo vya habari Nairobi, askofu huyo mstaafu wa kanisa la Methodist, alisema kuwa, “Maisha yana pandashuka za kushangaza. Kuna watu hata waliofungwa jela kisha baadaye wakainuka na kuvuka ng’ambo nyingine ya kisiasa.”

Bw Imathiu aliandamana na viongozi wengine wa jamii kutoka Mlima Kenya wakiwemo Askofu Bernard Kitungi, kamishna wa zamani Joseph Kaguthi, aliyekuwa waziri Bernard Ndotto, Canon Peter Karanja, miongoni mwa wengine.

Viongozi hao, waliwasihi Wakenya kumsaidia Bw Gachagua na familia yake kukabiliana na mabadiliko hayo yaliyowajia ghafla na kujipanga upya kwa amani.

“Tunamkumbuka aliyekuwa naibu rais na kumtakia kila la kheri pamoja na familia yake. Kumbuka mtu anapoacha ghafla kazi kama hiyo, huwa anahisi uchungu. Wakati mwingine familia hukabiliwa na wakati mgumu. Sisi ndio watu tunaohitajika kuwasaidia watu kama hao,” walisema kupitia taarifa ya pamoja.

“Huenda alikuwa na mapungufu yake lakini tunawasihi mumkumbuke na familia yake ili asijihisi mpweke. Tunaomba wabunge, maseneta na Wakenya, msimtupe bali mumsaidie kusonga mbele.”

Aidha, walimhimiza Bw Gachagua kujivunia alichofanikisha katika kipindi cha miaka miwili alichohudumu kama naibu rais na kumrai aunge mkono uongozi uliopo kwa maslahi ya Wakenya.

Viongozi hao walisema wanamuunga mkono Rais William Ruto, Naibu Rais mpya Kithure Kindiki na aliyekuwa naibu rais wakisema, “Tunawapenda wote. Wote ni watoto wetu. Gema imesema nyinyi ni wetu.”

“Na kwa sababu nyote watatu ni wetu, tunaomba wanaofanya kazi muwakumbuke ndugu zenu. Msiwatupe nje kwenye baridi,” walisema.

Aidha, walimshukuru Rais Ruto kwa kumteua Profesa Kindiki kumrithi Bw Gachagua, wakisema Dkt Ruto alihiari kumteua “mwana” mwingine kutoka eneo la Kati licha ya kuwa na uhuru wa kufanya kazi na yeyote kutoka maeneo mengineyo nchini.