Princess Jully aagwa akimiminiwa sifa kwa kuunganisha Wakenya kupitia ujumbe wa nyimbo
MAELFU ya waombolezaji mnamo Alhamisi, Novemba 7,2024 walifurika katika uwanja wa Bondo Nyironge, Suna Magharibi, kaunti ya Migori kumpa buriani mwanamziki maarufu wa mtindo wa Benga Julian Auma maarufu kama Princess Jully.
Mwanamziki huyo, aliyefahamika vyema kwa wimbo wake “Dunia Mbaya”, alifariki mnamo Oktoba,12, 2024 katika hospitali ya Migori alikokuwa akipokea matibabu baada ya kuugua kwa muda.
Wimbo huo ulivuma kati ya miaka 1990 na 2000 kutokana na maudhui yake ya kuhamasisha watu kujitahadhari dhidi ya zimwi hatari la ukimwi.
Mke wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, Bi Idah aliwaongoza wanasiasa, wasanii, maprodusa na waombolezaji wa matabaka mbali mbali kushuhudia safari ya mwisho duniani ya msanii huyo.
Waliopata nafasi ya kuhutubu katika mazishi hayo, walimmiminia sifa mwendazake kwa weledi wake wa utunzi wa nyimbo, wakisema mbali na kuwatumbuiza mashabiki, nyimbo zake nyingi zilikuwa zikielimisha na kufahamisha pia.
Gavana wa Migori Ochilo Ayacko alisema wanasiasa wanafaa kuunganisha Wakenya wote pasi na kuwagawanya jinsi msanii huyo alivyowaunganisha wapenzi wa muziki wake.
“Unaweza kuwa na mali nyingi lakini iwapo hutawaunganisha watu wako, jinsi alivyofanya mwanamziki huyo, hautakuwa na faida yoyote. Ndio maana tunatoa wito kwa viongozi kuunganisha watu wetu,” Gavana Ochilo alisema.
Mwenzake wa Homabay Gladys Wanga, naye alisema muziki wa Princess Jully utazidi kupendwa hadi na vizazi vijavyo kwa kuwa una mengi ya kuelimisha.
Seneta wa Migori Eddy Oketch, aliitaka serikali kuwakumbuka wasanii jinsi inavyowakumbuka raia wengine wanaoletea Kenya sifa kama vile wanariadha.