Lugha, Fasihi na Elimu

Shule ya Moi Girls Isinya ilivyoibuka washindi wa insha shindano la ‘Olive Seed Global Essay 2024’

Na FRIDAH OKACHI November 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WANAFUNZI wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Moi Isinya, Kaunti ya Kajiado waliibuka washindi kwenye shindano la uandishi wa insha la Olive Seed Global Essay 2024, lililofanyika mjini Narok.

Shindano hilo lilihusisha wanafunzi 450 wa gredi ya 11 na 12 katika shule 15 kutoka kaunti za Nairobi, Kajiado, Narok miongoni mwa kaunti zingine na walishiriki kuandika kuhusu changamoto wanazopitia.

Mkuu wa Shule ya wasichana ya Moi Isinya Bi Alice Saayo alijivunia wanafunzi wake kuwa waandishi bora katika shindano la insha ya Kiingereza nchini.

Alisema fursa hiyo itawapa jukwaa la kuonyesha talanta zao na kuchangia katika kupata suluhu kwa sababu ya kuzungumzia changamoto wanazopitia kama jamii na kujadili njia ambazo zinaweza kuwasaidia.

“Nawapongeza sana wasichana ambao wameweka shule yetu kwenye ramani leo. Tumeshinda kutokana na mazingira tuliyotengeneza shuleni kwa kuweka mtindo wa kusoma kila wakati. Pili, nafurahia wakfu wa Olive Seed kutoa msaada wa kuazisha maktaba na kuufadhili kwa maeneo ya watu wachache. Hili litasaidia vijana,” alisema Bi Saayo.

Mkurugenzi Mtendaji na mwazilishi wa Shirika la Olive Seed Bi Barbara McRenz alisema shindano la mwaka 2024 lililenga masuala yanayohangaisha vijana nchini.

Mkurugenzi Mtendaji na mwazilishi wa Shirika la Olive Seed Bi Barbara McRenz akizungumza na waandishi, Narok. Picha|Fridah Okachi

Shindano hilo likishirikisha vijana kueleza changamoto wanazopitia, walimu 17 walioteuliwa wakiangalia sarufi na maisha ya sasa.

“Insha hizo zilikuwa za kikweli kwa vile wanafunzi walizungumzia matatizo ya kiakili, utumiaji wa mitandao ya kijamii, dawa za kulevya na ukeketaji kwa wasichana kama matatizo wanayopitia,” alisema Bi Renz.

“Tulitumia mbinu hiyo ili kuona ni mradi upi ambao tutaweka kuwasaidia vijana hawa. Tunataka kujunuisha kwenye programu inayoendelea ya kila mwaka, kwa kuwapa fursa wajieleze zaidi,” aliongeza mwazilishi huyo.

Wasimamizi wa wakfu huo walitaka Wizara ya Elimu kuajiri washauri nasaha ili kutatua matatizo ya kiakili miongoni mwa wanafunzi nchini.

Bi Renz alipendekeza wizara itafute jinsi shule inafaa kuwa na mwongozo wa kutoa ushauri huo kwa watoto.

Miongoni mwa shule zilizoshiriki shindano hilo ni pamoja na shule za wasichana za Teresa’s Wamba, Namunyak, Buru buru, Ole Tipis, Sekenani, Maasai na shule ya wavulana ya Ololulung’a miongoni mwa nyingine.