Ruto aita tena mawaziri kuwasomea kuhusu utendakazi
RAIS William Ruto amewaita Mawaziri na Makatibu wote kufika Ikulu kutia saini kandarasi na kuweka malengo mapya ya miradi ya kutekeleza ambayo utawala wake unapatia kipaumbele huku akishinikizwa atimize ahadi alizotoa kabla ya uchaguzi.
Zoezi hilo, linalofanywa kila mwaka, limekuwa la kawaida tu lisilo na matunda ya kuonyeshwa huku washirika wake wakisema ni sehemu Muhimu cha Utendaji Kazi (KPI) kwa watumishi wa umma.
Katika barua ambayo Taifa Leo iliona, Mkuu wa Wafanyakazi na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei amewaamuru mawaziri na makatibu kufika binafsi Ikulu Jumanne, Novemba 19 kutia saini kandarasi za utendakazi.
Tukio hilo litakaloongozwa na Kiongozi wa Nchi linafuatia mazungumzo ya mwezi mzima kuhusu miradi muhimu itakayotekelezwa na kila wizara ifikapo Juni mwakani.
Mawaziri na makatibu – katika zoezi lililosimamiwa na Naibu Mkuu wa Wafanyakazi katika Ofisi ya Rais anayehusika na Utendakazi na Usimamizi wa Utekelezaji Serikalini, Bw Eliud Owalo, na Katibu wa Baraza la Mawaziri Bi Mercy Wanjau walijitolea kutimiza malengo kadhaa ndani ya kipindi hicho.
“Rais atasimamia utiaji saini wa kandarasi za utendakazi kwa wizara zote kwa Mwaka wa Fedha wa 2024/2025 katika Ikulu ya Nairobi Jumanne, Novemba 19, 2024 saa 9.00 asubuhi.
Mwanasheria Mkuu, Makatibu wote wa Baraza la Mawaziri na Makatibu Wakuu wote lazima wawepo katika hafla ya kutia saini,” akasema Bw Koskei kwenye waraka wa Novemba 12.
Wenyekiti na Maafisa Wakuu Watendaji wa Mashirika ya Serikali pia wamealikwa kuhudhuria hafla hiyo.
Bw Koskei alisema hafla ya kutia saini kandarasi hizo inaashiria hatua muhimu ya kufikia malengo ya maendeleo ya nchi pamoja na kuimarisha utendakazi na ufanisi wa utoaji wa huduma kwa umma.
Alitaja zoezi hilo kuwa kifaa kikuu cha usimamizi kinachorahisisha utekelezaji wa ahadi za kipaumbele za taasisi za umma kwa wakati, sambamba na kuimarisha uhusiano kati ya kupanga bajeti na utekelezaji wa majukumu yao.
“Kandarasi za utendakazi za Mwaka wa Fedha wa 2024/2025 zimejumuisha ahadi za kutoa ajenda ya maendeleo ya utawala wa Kenya Kwanza – Ajenda ya Mabadiliko ya Kiuchumi kuanzia mashinani (2022-2027).
Imetafsiriwa na BENSON MATHEKA