Kimataifa

Mfanyabiashara wa Tanzania aliyeponea kutekwa aongea: ‘Unene wangu uliniokoa’

Na THE CITIZEN November 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

DAR ES SALAM, Tanzania

DEOGRATIUS Tarimo, mfanyabiashara aliyeponea jaribio la kutekwa nyara na watu waliodai kuwa maafisa wa polisi mnamo Novemba 11, 2024 amesema nguvu na unene wake ndio ulimnusuru.

Kulingana na gazeti la The Citizen kisa hicho kilitokea katika mkahawa wa Rovenpic ulioko kitongoji cha Kiluvya, jijini Dar es Salama.

Kimeibua gumzo kali mitandaoni baada ya video kutokea ikionyesha wanaume wawili wakijaribu kumteka nyara Tarimo, maarufu eneo hilo kama Deo Bonge.

Picha za kamera za usalama (CCTV) zilimwonyesha mfanyabiashara huyo akivutwa na watu watatu kutoka mkahawa huo.

“Siwezi kusema ilikuwa ni mwili wangu mkubwa pekee, ila nguvu zangu pia zilinisaidia kwani ingekuwa rahisi kwao kunichukua,” Tarimo akaambia runinga ya Clouds kwenye mahojiano Novemba 13, 2024.

Baada ya kisa hicho, aliwasilisha ripoti kwa Kituo cha Polisi cha Gogoni.

“Niko sawa. Nilipoenda katika kituo cha polisi walinisaidia na sasa naendelea vizuri,” akasema.

Kwenye mahojiano na gazeti la Mwananchi mnamo Novemba 14, 2024 Tarimo alijizuia kutoa maeleza ya kina kuhusu kisa hicho lakini akasema hakuwatambua watu waliojaribu kumteka nyara.

“Kwa kweli sijajua ni akina nani, japo polisi wanakana kuwa hawakuwa wenzao. Tulipowahoji walidai kuwa maafisa wa polisi lakini hawakutuonyesha vitambulisho vyovyote,” akaeleza.

Watu walioshuhudia kisa hicho, wakiwemo mhudumu mmoja wa hoteli, alieleza jinsi watekaji hao walijitambulisha kuwa maafisa wa polisi kutoka Gogoni na wakaamuru kuwa Tarimo aingie katika gari aina ya Toyota Raum waliosafiria kufika hapo.

Ripoti zingine zinasema kuwa Tarimo amekuwa akiwasiliana na watu waliojaribu kumteka nyara mnamo Oktoba 25, 2024, na wakaagana kukutana mnamo Novemba 11 kwa mazungumzo ya kibishara.

Alipouliwa ikiwa amekuwa akijadiliana nao kabla ya kukutana, Tarimo alisema suala hilo linachunguzwa na polisi wakati huu.

“Ni kweli, lakini haya ni mambo yanayochunguzwa na polisi. Nadhani tunapaswa kuwaacha wakamilishe kazi yao kisha wawasilishe ripoti kamili, kwani kutoa maelezo kinzani kunaweza kuleta shida.”

Mnamo Novemba 13, 2024 msemaji wa polisi David Misime alitoa taarifa akiwahakikisha umma kwamba wanawafuatilia waliohusika na jaribio hilo la utekaji nyara.

IMETAFSIRIWA NA CHARLES WASONGA