Maoni

Jamii ishirikishwe kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa kongamano likiendelea nchini Azerbaijan

Na MARY WANGARI November 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

AWAMU ya 29 ya kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu Hali ya Anga, Cop29, ilianza rasmi Jumatatu Novemba 11, 2024 katika jiji kuu la Baku, nchini Azerbaijan.

Viongozi na wajumbe wa mataifa takriban 200 wamejumuika katika kongamano hilo la wiki mbili, linalokusudiwa kutoa nafasi ya mdahalo muhimu kuhusu ushirikiano katika uwekezaji wa kupunguza viwango vya joto duniani.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, afisa anayesimamia masuala ya hali ya anga katika Umoja wa Mataifa  (UN), Simon Stiell, alihimiza viongozi wa dunia kuimarisha uhusiano.

Alionya kuwa, kila nchi itagharamia ikiwa mataifa machache yatapuuza mikakati ya kuzuia viwango vya joto kupanda kupita kiasi.

Kongamano hili lilianza siku chache tu baada ya Amerika kumrudisha madarakani, Donald Trump, ambaye ameapa kuiondoa Amerika katika mkataba wa Paris, kuhusu kupunguza viwango vya joto duniani.

Katika miaka ya hivi karibuni, imezidi kubainika kuwa nchi zinazoendelea, hususan barani Afrika Kenya  ikiwemo, zinachangia padogo katika kuzorotesha hali ya anga lakini ndizo wahasiriwa wakuu, kila yanapotokea majanga yanayosababishwa na athari hasi za hali ya hewa.

Mataifa makuu duniani kutoka Magharibi na Uropa ambayo yameendelea kiviwanda yamechangia zaidi ongezeko la viwango vya joto vinavyozidi kupanda na kutishia hatima ya dunia.

Huku wataalamu wakionya kwamba viwango vya joto vitavuka kiwango kinachohitajika mwaka huu, baadhi ya mataifa makuu duniani yameonyesha kulegeza azma yake na kuhatarisha zaidi mataifa maskini.

Kurejea kwa Trump kwa kishindo kumezua hofu kwamba, mataifa makuu hayatakuwa na motisha wa kushiriki mazungumzo kuhusu muafaka wa Paris.

Uhalisia huu umejitokeza bayana baada ya viongozi wachache tu wa mataifa makuu duniani almaarufu G20, yanayochangia karibu asilimia 80 ya hewa inayochafua mazingira, kujitokeza kuhudhuria COP29 jijini Baku.

2024 ni moja kati ya miaka ambayo imegubikwa na majanga ya kuhofisha, kuanzia mafuriko, maporomoko ya ardhi, na kiangazi cha muda mrefu na mengineyo, huku nchi maskini zikiathirika zaidi. Japo suala la mabadiliko ya hali ya anga ni uhalisia usioweza kupuuziliwa mbali, imedhihirika kuwa idadi kubwa ya wanajamii nchini, hasa mashinani, wangali gizani kuhusu mikakati ya kudhibiti hali ya anga.

Hali hii imesababisha wanajamii kuchelea kujihusisha na miradi ya uwekezaji katika soko la kaboni kwa kukosa ufahamu.