Maswali tele kuhusu mauaji ya wanawake
MNAMO Julai mwaka huu, 2024 wanachama wa Shirika la Kijamii la Mukuru Community Justice Centre waliopoa magunia yaliyojaa sehemu za miili ya binadamu kutoka kwa timbo la Kware lililojaa maji katika kitongoji duni cha Mukuru Kwa Njenga.
Waliendesha zoezi hilo bila vifaa vya kujikinga.
Miezi kadhaa baadaye, mashirika kadha ya eneo hilo yanahisi kutelekezwa na asasi mbalimbali ambazo awali zilifika hapo kufuatilia habari kuhusu kuuawa kwa wanawake na sehemu za maiti yao kutupwa ndani ya timbo hilo.
Mashirika hayo sasa yanaitaka serikali kuchukua hatua zaidi.
“Jamii za hapa hazijarejelea maisha ya kawaida kufuatia tukio hilo lakini inaonekana kuwa serikali imeacha kufuatilia suala hilo,” akasema Anami Daudi Toure, mwenyekiti mwenza Mukuru Community Justice Centre.
Mnamo Jumatano, shirika hilo lilitoa ripoti iliyosheheni maelezo kuhusu hatua iliyochukua kufuatia mauaji ya Kware; kuanzia kuwaleta watu walioopoa miili kutoka kwa maji taka hadi kutoa usaidizi kwa familia za waathiriwa.
Ripoti hiyo inahojia hatua zilizochukuliwa na serikali, polisi, makundi ya kitaifa kutetea haki na vyombo vya habari huku ikitoa taaswira ya jamii iliyotelekezwa na kuachiwa mzigo wa kushughulikia madhara ya tukio hilo pekee yao.
Wanashikilia kuwa hatua kutoka kwa serikali haijakuwa ya kuridhisha.
“Mshukiwa mkuu anafaa kukamatwa tena na kufunguliwa mashtaka kortini. Aidha, tunahitaji kutambua miili yote iliyotolewa kutoka Kware na tunahitaji kujua maelezo kuwahusu,” akasema Toure.
Ni wanawake sita pekee wametambuliwa kutokana na mabaki kadhaa ya miili iliyoopolewa kutoka kwa timbo hilo.
Wao ni; Roseline Akoth, Josephine Mulongo, Christine Mwende, Wilkister Ososo, Brenda Shatuma na Imelda Karenya.
Wanachama wa Mukuru Community and Justice Centre wanaamini kuwa miili mingi bado haijapatikana na kwamba shughuli ya uopoaji ilisitishwa mapema.
Ripoti hiyo inaelezea jinsi serikali ilivyofeli kutambua waathiriwa wote kwa kutumia data ambazo inahifadhi.
“Huenda hii ndio maana kuna idadi kubwa ya miili, isiyotambuliwa, katika hifadhi ya maiti ya City,” akasema Geoffret Mboya, ambaye ni mwanaharakati anayehudumu katika shirika hilo.
Julai 25, polisi walimkamata Collins Jumaisi, 33, anayedaiwa kukiri kuangamiza wanawake 42 tangu mwaka wa 2022, akiwemo mkewe.
Lakini baadaye wakili wa mshukiwa huyo alisema kuwa mteja wake alitoa madai hayo baada ya kulazimishwa kufanya hivyo.
Agosti 11, Jumaisi alitoroka kutoka Kituo cha polisi cha Gigiri, Nairobi akiwa na washukiwa wengine 12 raia wa Eritrea na kuibua maswali kuhusu mienendo ya polisi. Hajapatikana hadi kufikia sasa.