Raila akemea wabunge na kuunga magavana kuhusu mgao kwa kaunti
KINARA wa ODM Raila Odinga ameunga Seneti kutaka serikali za kaunti zitengewe Sh400 bilioni huku akishutumu Bunge la Kitaifa kwa kuhujumu ugatuzi.
Bunge la Kitaifa na Seneti kwa sasa zinavutana vikali kuhusu mgao kwa serikali zote za kaunti 47. Maseneta wanataka kaunti zimegewe Sh400 bilioni huku Wabunge wakipendekeza Sh380 bilioni.
Mzozo kuhusu tofauti ya Sh20 bilioni umeendelea hata baada ya kuundwa kwa kamati ya upatanishi ya wanachama 18 ambayo inajumuisha wanachama sawa kutoka mabunge hayo mawili.
Bw Odinga alisema inashangaza kwamba, Bunge lilikuwa likishinikiza kupunguza kiwango cha pesa za mgao wa kaunti. Alilinganisha hatua ya wabunge hao na kunyonga kaunti na kuziua pole pole.
Alisema sheria inatengea kaunti angalau asilimia 15 ya Mapato ya Kitaifa na kusema Sh400 bilioni zilizopendekezwa na Seneti zinawakilisha asilimia 15 ya Mapato ya Kitaifa.
Alisema Bunge lilipendekeza marekebisho ya Sheria ya Ugavi wa Mapato, ambapo wanapendekeza Sh380 bilioni kwa kaunti, tofauti na Sh400 bilioni ambazo tayari zimeainishwa kwenye Sheria ambayo inatumika kwa sasa.
‘Msukosuko wa sasa na majaribio ya kupunguza mgao unaonyesha hatari ya kurudisha nyuma ugatuzi. Ninawaomba wabunge wetu wawe wawezeshaji wa ugatuzi na kukataa kushirikiana na wale wanaoazimia kuua ugatuzi,” akasema Bw Odinga.
Akihutubia wanahabari Ijumaa katika afisi yake ya Nairobi, Bw Odinga aliwataja Wabunge kama wachoyo kwa jaribio lao la kudhibiti mgao wa kaunti huku wakati huo huo wakimezea mate pesa zaidi kuwa chini ya usimamizi wao.
Waziri Mkuu huyo wa zamani alifichua kuwa, mbali na kudhibiti Hazina ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF) na Hazina wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Usawa, wabunge walikuwa wakipanga njama ya kudhibiti Hazina ya Ushuru wa Kukarabati Barabara (RMLF).
Aliwashutumu wabunge hao kwa kutaka kuanzisha, kutekeleza miradi na kuisimamia kwa wakati mmoja.
Alisema “utekelezaji wa miradi haujawahi kuwa na kamwe hauwezi kuwa kazi ya wabunge bila kuleta mgongano mkubwa wa uwajibikaji katika mfumo wetu wa utawala kwa hasara yetu sote.”
Alisema ni aibu kuwa, baadhi ya wabunge hao wenyewe ni wanakandarasi katika miradi inayofadhiliwa na NG-CDF.’Ukweli usiofichika ni kwamba, mzozo huu ni kuhusu kunyakua mamlaka na kuhujumu katiba,’ alisema Bw Odinga.
“Bunge linatunga sheria, na kuhakikisha sheria zinatekelezwa na kufuatwa. Ni kutokana na hali hii ambapo mzozo unaoendelea kati ya mabunge yetu mawili kuhusu mgao wa mapato ukiwa tisho, haufai na hauhitajiki.
Katiba tuliyoizindua mwaka wa 2010 inaelekeza jinsi serikali na nchi yetu inavyofanya kazi,” alisema.
Alisema mzozo huo tayari unatishia kusimamisha shughuli na utoaji wa huduma katika kaunti. Alisema kaunti tayari zina matatizo na haziwezi tena kufadhili huduma muhimu.
“Bunge la Kitaifa linajitahidi kupunguza mgao wa mapato kwa kaunti, kwa kupuuza kabisa katiba na mapendekezo ya Seneti. Hatua hii sio tu kinyume cha sheria na kinyume cha katiba, bali inaweka historia hatari sana ambayo, ikiruhusiwa , itasababisha kukabwa koo polepole lakini kwa uthabiti na hatimaye kuua kaunti,” akasema.
Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Ahmed Abdullahi Alhamisi alisema mzozo huo unaendelea kuumiza kaunti, huku shughuli zikikwama kwani pesa zinazotarajiwa kutoka kwa serikali ya kitaifa zimecheleweshwa
.’Ninataka Wakenya wajue kuwa kaunti ziko kwenye shida, haziwezi kufanya maamuzi, haziwezi kukamilisha michakato ya bajeti kwa sababu ya ukosefu wa Sheria ya Ugavi wa mapato kwa Kaunti,’ alisema Bw Abdullahi.
IMETAFSIRIWA Na BENSON MATHEKA