Askofu Mkuu Ole Sapit sasa aiponda serikali aliyoishabikia awali
KANISA la Kianglikana Nchini (ACK) sasa limejitokeza waziwazi na kusema linaunga mkono kauli ya Maaskofu wa Kanisa Katoliki serikali ya Kenya Kwanza inaendesha nchini visivyo huku ikikosa kutimiza ahadi zake kwa raia.
Kanisa hilo limekana habari zilizochapishwa kwenye gazeti moja la humu nchini kwamba halikubaliani na msimamo wa maaskofu hao chini ya Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Nchini (KCCB).
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumatatu, Novemba 18, 2024 kiongozi wa kanisa hilo Askofu Mkuu Jackson Ole Sapit aliwasuta viongozi wa kisiasa waliokosoa kauli ya maaskofu hao akiwataja kama “wanafiki”.
“Tunaamini kuwa serikali haijaboresha taifa hili kwa kulielekeza mkondo mzuri. Kwa hivyo, wanasiasa waliowasuta maaskofu na kupuuzilia taarifa yao wakiitaja kama ya ‘uwongo, inayopotosha na isiyo sahihi’ ndio waongo kabisa! Maaskofu hao wameongea yaliyo yaliyomo moyoni mwa Wakenya wote na kueleza ukweli ulivyo,” akasema Ole Sapit.
Akaongeza: “Hamna mashambulio na vitisho vitakavyolizuia Kanisa la Mungu kulaani maovu na kuwaambia ukweli walioko mamlakani.”
Askofu Mkuu Ole Sapit aliwataka wanasiasa na wale walioko serikalini kukubali kuwa mambo sio shwari nchini na wakome kuendeleza mtindo wa kudharau sheria.
Hata hivyo, kiongozi huyo wa ACK ni mmoja wa wale waliounga mkono ushindi wa Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2022.
Mnamo Agosti 15, 2022, Ole Sapit alikuwa mstari wa mbele katika Ukumbi wa Bomas akimshinikiza aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati atangaze “upesi” matokeo na amtawaze Dkt Ruto kama mshindi halali licha ya malalamisha kutoka kwa wafuasi wa Azimio.
Dakika chache baada ya baraza la KCCB kuisuta serikali kwa kuendeleza “mwenendo wa kutoa kauli za uwongo”, Rais William Ruto na mawaziri na wanasiasa watetezi wa serikali walijitokeza na kupinga kauli hiyo.
Akiongea alipoongoza hafla ya kufuzu katika Chuo Kikuu cha Tangaza, Rais Ruto aliwaonya maaskofu hao dhidi ya kutoa kauli alizozitaja kama zisizo za kweli “kwani kauli kama hizo zinaweza kuwaathiri nyinyi wenyewe baadaye.”
Nao mawaziri Julius Ogamba (Elimu), mwenzake Debra Mulongo Barasa (Afya) na Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja waliwakashifu maaskofu hao kwa “kupotosha umma”.
Baraza la KCCB lilisema utekelezaji wa mtaala mpya wa CBC hauendeshwi vizuri sawa na mfumo mpya wa ufadhili wa msomo katika vyuo vikuu.
Aidha, walikosoa utekelezaji wa Bima mpya ya Afya ya Kijamii (SHIF) wakiisuta serikali kwa kufeli kulipa madeni kwa hospitali zinazomilikiwa na mashirika ya kidini kutokana na NHIF.
Aidha, maaskofu hao waliiponda serikali kuwa kutumia maafisa wa polisi kuendeleza vitendo vya ukiukaji wa haki za kibinadamu kama utekaji nyara wa watu wanaosawiriwa kuwa wakosoaji wake.