Ndindi Nyoro, Wamuchomba nje Ruto akianza kufagia wabunge wasioshabikia serikali
MBUNGE wa Molo Kuria Kimani atarithi nafasi ya mwenzake wa Kiharu Ndindi Nyoro kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti kwenye Bunge la Kitaifa wiki hii.
Duru zimeeleza Taifa Leo kuwa kutakuwa na mabadiliko yatakayotekelezwa katika kamati mbalimbali za bunge ambapo wabunge 13 wanaoonekana hawashabikii serikali watatimuliwa.
Watakaoonyeshwa mlango ni wandani wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua huku wandani wa Kinara wa upinzani Raila Odinga ambaye kwa sasa ni msingi wa utawa wa Kenya Kwanza, wakitunukiwa nafasi za hadhi.
ODM itapokezwa uenyekiti wa Kamati ya Fedha na Mipango ambayo imekuwa ikishikiliwa na Bw Kimani. Japo kwa kawaida mabadiliko hayo hukumbatiwa wakati wa mkutano wa wabunge wa chama husika, hakuna mkutano wa wabunge wa Kenya Kwanza ambao umeratibiwa wiki hii.
Hii inaashiria kuwa suala hilo limeidhinishwa na sasa ni kazi ya Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah na mwenzake wa wachache Junet Mohamed kuarifu Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula.
Haya yanafanyika wakati ambapo Rais William Ruto naye anatarajiwa kutoa hotuba yake ya kila mwaka kwa wabunge mnamo Alhamisi wiki hii.
Walikuwa majemedari wa Ruto
Bw Nyoro alikuwa kati ya wabunge ambao walikuwa majemedari na wandani wa Rais Ruto kabla na baada ya uchaguzi wa mnamo 2022.
Hata hivyo, inaonekana ametengana na serikali hasa baada ya kukataa kuchukua msimamo wakati ambapo Bw Gachagua alikuwa akitimuliwa bungeni mwezi uliopita.
“Kilichomchongea Nyoro ni kuwa aliamua kukimya wakati ambapo alihitajika na akamsaliti Rais,” akasema mbunge mmoja huku akikisia kuwa huenda mbunge huyo akaachwa nje kabisa au kupewa wadhifa wa kamati isiyokuwa ya hadhi.
Bw Nyoro anayehudumu muhula wa pili pia hakuwa bungeni wakati ambapo kura ilikuwa ikipigwa ya kumn’oa Bw Gachagua mnamo Oktoba 8.
Bw Ichung’wah ambaye ana jukumu la kuwaweka wabunge kwenye kamati mbalimbali amekuwa akisema kila mara kuwa mabadiliko yananukia na wale ambao hawahudhurii vikao vya bunge watatimuliwa afisini.
“Utaondolewa mamlakani kama mwenyekiti wa kamati kama hauhudhurii vikao vya bunge. Lazima uwe bungeni kila wakati na kuepushia Spika kazi ngumu ya kuwaita wabunge waje wahudhurie vikao,” akasema Bw Ichung’wah.
Kando na Bw Nyoro wabunge wengine waasi kwa serikali ambao watatimuliwa kwenye kamati mbalimbali ni Gathoni Wamuchomba (Githunguri), George Kariuki (Ndia), James Gakuya (Embakasi Kaskazini), Johana Ng’eno (Emurua Dikir), Vincent Musyoka (Kawi) na Wanjiku Muhia (Kipipiri).
Walipinga kumtimua Gachagua
Wabunge wengine ni Nimrod Mbai (Kitui Mashariki) na Kareke Mbiuki (Maara) ambao pia walipinga hoja ya kumtimua Bw Gachagua.
Bi Wamuchomba alikosana na utawala wa Kenya Kwanza mwaka wa kwanza wa uongozi wake naye Bi Muhia pia alijichongea kwa kutounga hoja ya kumbandua Bw Gachagua.
Bw Ndia naye hajakuwa akihudhuria vikao vya bunge licha ya kuwa ni mwenyekiti wa kamati ya uchukuzi na miundomsingi. Bw Gakuya ambaye yupo katika kamati ya uchukuzi kama mwanachama wake ni mwandani wa Bw Gachagua.
Rais Ruto anaonekana kuwa na uaminifu wa juu kwa Bw Kimani kutokana na ukakamavu wake wa kutetea serikali ndani na nje ya bunge.
Boma la Bw Kimani lilivamiwa na kuharibiwa kisha mali yake kuporwa wakati wa maandamano ya Gen Z kutokana na jinsi alivyopigia debe na kuunga Mswada wa Fedha 2024 uliopendekeza nyongeza kubwa ya ushuru.
Serikali Jumuishi
Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa, naibu mwenyekiti wa kamati ya uchukuzi na miundomsingi alisema kuwa mabadiliko hayo ni lazima hasa wakati ambapo bunge lipo katikati ya muhula wake wa kudumu.
“Tuna serikali jumuishi ambayo uwakilishi wake lazima nao uonekane kwenye uongozi wa kamati za bunge. Hii ndiyo sababu kuu ya uongozi wa kamati mbalimbali kufanyiwa mabadiliko,” akasema Bw Barasa.
Kamati za kawi, bajeti, fedha, biashara na nyumba ni kati ya zile za hadhi ambazo wabunge hupigania sana kuongoza au kuwa wanachama kutokana na majukumu yao yanayowavunia marupurupu kadhaa.
Imetafsiriwa na Cecil Odongo