Wimbi la mabadiliko Kiongozi wa Upinzani akiibuka mshindi wa urais Somaliland
HARGEISA, SOMALILAND
WIMBI la mabadiliko ya kisiasa barani Afrika jana lilitua Somaliland baada ya upinzani kuonyesha serikali kivumbi kikali kwenye uchaguzi wa urais.
Rais Musi Bihi Abdi alibwagwa na kiongozi wa upinzani Abdirahman Mohamed Abdullahi kwenye uchaguzi wa taifa hilo ambalo lilijitenga na Somalia tangu 1991.
Bw Abdullahi alikuwa akiwania kiti hicho kupitia chama cha Waddani na alipata asilimia 64 ya kura kulingana na matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Somaliland (NEC).
Wapiga kura nchini humo waliingia debeni wiki jana katika uchaguzi ambao ulifanyika baada ya kucheleweshwa kwa miaka miwili kutokana na ukosefu wa fedha na sababu nyinginezo.
Rais Abdi alikuwa akisaka kuongoza kwa muhula wa pili baada ya kuwa afisini kwa kipindi cha miaka saba. Alijizolea asilimia 35 ya kura kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na NEC.
Wawaniaji wote wawili wakati wa kampeni waliahidi kufufua uchumi ambao upo pabaya na pia kushinikiza taifa hilo litambuliwe sana na jamii ya kimataifa.
Kusambaratishwa
Somaliland ambayo ilipata uhuru wake mnamo 1991 wakati ambapo Somalia ilikuwa ikielekea kusambaratiswa na vita, imejijengea mazingira yanayoridhisha kisiasa na kidemokrasia.
Hii ni kinyume na majirani wao Somalia ambao wamekuwa wakitatizwa na uhasama pamoja na vuta nikuvute kati ya viongozi, nchi hiyo ikikosa kabisa uthabiti wa kisiasa.
Mbali na kuwa na serikali yake, Somaliland ina sarafu yake na pia muundo unaotambulika wa kiusalama na kijeshi.
Changamoto kubwa zaidi kwa raia wake ni kuwa taifa hilo halijatambuliwi na nchi yoyote ulimwenguni.
Kukosa huko kutambuliwa kumeinyima nchi yenyewe mwanya wa kupata mikopo na raia wake milioni sita hawana uwezo wa kusafiri hadi mataifa mengine.
Makao yake makuu ni jiji la Hargeisa na nchi hiyo inapanga kuingia kwenye mkataba na Ethiopia ili iweze kutumia bandari yake. Mkataba huo ukifaulu, basi Ethiopia itatambua Somaliland kama taifa kivyake.
Hasira kutoka kwa Somalia
Hata hivyo, mkataba huo umeibua hasira kutoka kwa Somalia ambayo inaona hatua hiyo kama ya uchokozi na inayolenga kulemaza nia yake ya kudhibiti Somaliland.
Ethiopia imekuwa mstari wa mbele katika kushiriki juhudi za kuleta amani Somalia kwa kuisaidia kupambana na makundi ya kigaidi yaliyojihami vikali.
Nchi za Misri na Eritrea ambazo zimekuwa na uhasama mkubwa na Ethiopia zinapinga mkataba wa taifa hilo na Somalilanda kuhusu matumizi ya bandari.
Hatua hiyo imefanya Misri na Eritrea kuwa washirika wa Somalia ambao pia wanapinga mkataba huo.
Kufuatia kuchaguliwa kwa Rais Donald Trump, Somaliland ina imani kuwa Amerika itatambua uhuru wao wa kuwa taifa kivyake.
Hii ni kwa sababu maafisa wa serikali wa Amerika waliohudumu wakati wa muhula wa kwanza wa Rais Trump kati ya 2016-2020 waliweka wazi kuwa wanatambua uhuru wa Somaliland.