Wapemba waliobadili majina wahangaika kupata uraia wa Kenya
BAADHI ya watu wa jamii ya Wapemba, wamefichua matatizo wanayopitia kujisajili rasmi kama Wakenya.
Mwaka uliopita, Rais William Ruto aliidhinisha jamii hiyo kuwa mojawapo ya makabila yanayotambuliwa kama Wakenya.
Hatua hiyo ilinuiwa kuwafungulia nafasi Wapemba kupata stakabadhi muhimu kama vile vitambulisho vya kitaifa na vyeti vya kuzaliwa ili wapokee huduma sawa na raia wengine wa Kenya.
Imebainika kuwa, wengi wao walipoingia nchini kuanzia miaka ya sitini, waliamua kutumia majina ya makabila ya humu nchini ili kurahisisha uwezo wao wa kutochukuliwa kama raia wa kigeni.
Hata hivyo, baada ya serikali kuamua kwamba Wapemba watambuliwe kama Wakenya, wanajamii hao wamekuwa wakijaribu kutafuta vyeti na vitambulisho kwa majina yao halisi lakini wanatatizika.
Mmoja wao, Bw Dida Hamadi Makame, alieleza kuwa ameshindwa kurejelea jina lake halisi kwani mwaka wa 1986 alikuwa amebadilisha jina lake liwe Dida Hamisi Idi.
“Watoto wangu huniuliza watafanyaje, kwani sisi ni Wapemba na wanahitaji kujisajili kupokea vitambulisho. Nilimwambia mmoja wao atumie jina lolote analotaka ili aache kutatizika,” akasema.
Bw Abdul Mohamed Mbarari, ambaye pia ni wa kutoka katika jamii hiyo, alisema kuna baadhi yao walipewa vitambulisho mwaka uliopita katika hafla iliyoongozwa na rais mjini Kilifi, lakini hawawezi kuvitumia.
Maelezo yaliyo kwenye vitambulisho
Bw Mbarari alisema, maafisa wa serikali huwaambia maelezo yaliyo kwenye vitambulisho hivyo hayapatikani katika sajili ya watu kitaifa.
Naibu Katibu wa Wapemba nchini Omar Kombo, alithibitisha haya na kusema ingawa serikali ilionyesha nia ya kutatua ukosefu wa uraia kwa jamii hiyo, kuna baadhi yao bado hawatambuliwi kuwa Wakenya.
“Jamii ya Wapemba itaendelea kukosa uraia ikiwa baadhi yetu bado hawatambuliwi,” akaeleza.
Ijumaa iliyopita, katika hafla ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu Wapemba wapewe uraia nchini, Mbunge wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya, alisema masaibu hayo yanasikitisha.
Alirai serikali itume maafisa husika kukita kambi katika maeneo ya Pwani ambako Wapemba hupatikana, ili kutatua hali hiyo.
“Tunataka suala hili litatuliwe mwaka huu ili ifikapo 2025, kusiwe na Mpemba yeyote ambaye atanyimwa huduma katika benki na pia waweze kujisajili kwa bima ya kijamii ya afya (SHIF),” akasema.
Katibu wa Uhamiaji na Huduma za Raia Julius Bitok, alitoa hakikisho kwamba serikali imejitolea kuhakikisha Wapemba wanapokea huduma zote nchini sawa na raia wengine wa Kenya.
Umoja wa Mataifa hukadiria kuna Wapemba karibu 7,000 nchini.
Kulingana na serikali, zaidi ya 6,000 walishasajiliwa kuwa Wakenya rasmi.