Salamu spesheli ya ‘Toto’ ilivyozua cheche bungeni
WABUNGE wanawake Jumanne Novemba 19, 2024 walilalamika vikali kiongozi wa wachache Junet Mohamed alipopendekeza kuwa wanawake wawe wakiwasalimu wanaume wakiwa wamepiga magoti.
Waliongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Kisii Dorice Donya aliyedai pendekezo hilo linaweza kuvunja taasisi ya ndoa na kusambaratisha familia.
“Hilo pendekezo la Junet ni baya kwani linaweza kuvunja ndoa, wanaume watakuwa wakishikiniza kuwa wanawake wapige magoti mbele yao kila mara. Napendekeza kuwa wanaume ndio wawe wakiwapigia magoti wanawake kama ishara ya kuwaonyesha upendo,” akasema.
Mjadala huo uliibuka baada ya Kiranja wa Wachache Millie Odhiambo kulalamika kuwa haikuwa sawa kwa Mbunge Mwakilishi wa Bomet Linet Chepkorir almaarufu Toto, kupiga magoti akimsalimia Mbunge wa Sotik Francis Sigei.
“Mheshimiwa Spika sio sawa kwa Mheshimiwa Toto kumsalimia Bw Sigei akiwa amepiga magoti. Hata ikiwa hatua hiyo inakubalika katika mila na tamaduni zao kule Bomet kuashiria heshima kwa wakubwa, hapa bungeni wabunge wote wako na hadhi sawa,” akasema Mbunge huyo wa Suba Kaskazini.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Mheshimiwa Toto kufika Bunge baada ya likizo ya uzazi.
Lakini Bw Junet, ambaye ni Mbunge wa Suna Mashariki, alitofautia na Bi Odhiambo akisema Bi Toto anaiga mtindo ulioko Uganda ambako “wanawake hupiga magoti mbele ya wanaume”.
“Hivyo ndivyo inapasa kuwa hapa bungeni na hata kule nje. Wanawake wanafaa kuonyesha wanaume heshima,” akaeleza.
Spika Wetang’ula naye alionekana kuunga mkono kauli ya Bw Junet aliposema kuwa anakotoka “wanawake hupiga magoti mbele ya wanaume kama ishara ya heshima”.
“Kule ambako mimi na Jack Wamboka tunatoka ni jambo la kawaida kwa wanawake kupiga magoti mbele ya wanaume. Na hiyo ni ishara ya heshima na hatujaona ndoa zikivunjika wala familia zikisambaratika,” akaeleza huku wabunge wanawake wakipaza sauti wakisema “hapa, hapa….. hiyo haiwezekani, sisi sio watumwa.”
Bw Wetang’ula na Bw Wamboka, ambaye ni Mbunge wa Bumula wanatoa kaunti ya Bungoma, iliyoko magharibi mwa Kenya.