Kimataifa

Kiongozi wa upinzani Uganda Kizza Besigye atekwa nyara Nairobi, mkewe asema anazuiliwa na jeshi Uganda

Na BENSON MATHEKA November 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KIONGOZI wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye alitekwa nyara akiwa Kenya mwishoni mwa wiki jana.

Mkewe anasema mumewe alitekwa nyara jijini Nairobi, Kenya na sasa anazuiliwa katika jela la kijeshi nchini Uganda.

Katika ujumbe aliochapisha kwenye X, Winnie Byanyima, mkewe Besigye alisema kwamba mumewe alikamatwa katika mji mkuu wa Kenya Nairobi Jumamosi wakati wa hafla ya uzinduzi wa kitabu cha kiongozi wa upinzani Martha Karua.

“Sasa nimefahamishwa kuwa yuko katika jela la kijeshi Kampala,” alisema, akiitaka serikali ya Uganda kumwachilia mumewe.

Besigye, 68, anaongoza chama cha kisiasa cha Forum for Democratic Change (FDC) na aligombea urais na kushindwa mara nne na Rais Yoweri Museveni, ambaye amekuwa madarakani tangu 1986.

“Sisi familia yake na mawakili wake tunataka kumuona,” mkewe aliandika kwenye X na kuongeza kuwa: “Yeye si mwanajeshi. Kwa nini anazuiliwa kwenye jela la kijeshi?”

Winnie Byanyima ni mtetezi wa haki za binadamu na mkurugenzi mtendaji wa Unaids, mpango wa pamoja wa Umoja wa Mataifa ambao ulianzishwa ili kupiga vita Ukimwi.

Kizza Besigye aliwahi kuwa daktari wa kibinafsi wa Museveni kabla ya kutofautiana naye na kukumbatia siasa za upinzani.

Kiongozi huyo wa upinzani amekamatwa mara kadhaa miaka ya awali.

Wakati mmoja alipigwa risasi mkononi, na mwingine alipata majeraha ya macho baada ya kumwagiwa dawa yenye mwasho.

Kutekwa nyara kwake kunafuatia kisa cha Julai 23 cha kukamatwa kwa wanaharakati 36 wa Uganda wanaohusishwa naye mjini Kisumu kabla ya kusafirishwa hadi Uganda.

Wanaharakati hao wa kisiasa walitekwa nyara na kusafirishwa hadi Uganda ambako walifunguliwa mashtaka ya uhaini na kupelekwa katika Gereza la Kitalya.

Wanaharakati hao ambao waliachiliwa kwa dhamana hivi majuzi, walikana mashtaka hayo na kusema walikuwa wakihudhuria warsha walipokamatwa.

Wanaharakati hao 36 wanadai kuteswa wakati wa kuzuiliwa kwao.