Maoni

MAONI: Rais asikie sauti ya maaskofu kwa kuwa hawaropokwi ovyo

Na PAUL NABISWA November 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NILIFURAHIA ghaya matamshi ya kanisa Katoliki kupitia kwa kongamano la maaskofu wao kuwa serikali ya Rais William Ruto inaogolea katika bahari kuu ya uongo.

Sisemi hivyo kwa kuwa nilikuwa mtoto misa kwa miaka minane, la. Sisemi hivyo kwa sababu najua kupiga ishara ya msalaba, hapana. Wala sizungumzi hayo kwa kuwa nimesoma rozari takatifu kwa miaka mingi na kukariri sala ya Salaam Maria, la.

Kanisa Katoliki limesema kuwa Rais amejenga mkururo mrefu wa hadaa kwa Wakenya kuhusu utekelezaji wa miradi ya serikali. Yaani mfumo wake wa serikali unataka Wakenya wote wapige makofi ya shangwe kuwa SHA ni mufti na SHIF ndio dawa tosha kwa wagonjwa. Mashabiki wa Rais wakawataka maaskofu kujali namna ya kukomaza imani ya Wakenya. Ndio viongozi wetu hao.

Rais amekiri kuwa kuna jambo. Mbele ya maaskofu huko Embu akasema anatafuta kanisa atakalohudhuria misa Jumapili. Akajumuika na wenzake katika kanisa Katoliki la Soweto, Jumapili. Bila shaka akitoka huko atakuwa amejua kukariri sala fupi ya “Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu kama mwanzo na sasa na siku zote na milele, Amina.” Baada ya hapo atawauliza mawaziri wake, huko nje watu wanasema mimi ni nani? Wakishajibu, atawauliza na nyinyi mnasema mimi nani? Jibu unalo.

Maaskofu hawa hawakukurupuka na kuropoka. Wanakutana na waumini wao katika ngazi za majimbo na parokia. Mapadri wamekutana na waumini wao wakiungama dhambi zao. Na inawezekana hata baadhi ya waumini wamewaambia mzigo wanayobebeshwa na hii serikali “tukufu” ya Rais Ruto.

Msimamo wa maaskofu hao ni sauti ya Wakenya wengi. Wameonekana kuchukua nafasi walizochukua hayati Alexander Muge, Henry Okulu na David Gitari katika miaka ya themanini na tisini. Wanaendeleza kauli alizotoa Askofu Timothy Njoya ambaye alipata kipigo cha nyoka miaka ya tisini akitaka katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa 1997.

Wakifanya hivi wakati huu tunamkumbuka aliyekuwa askofu wa jimbo la Nakuru wa Kanisa Katoliki Ndigi Mwana a’Nzeki ambaye alitangaza kuwa mapigano ya kikabila yalikuwa yameshika kasi katika uliokuwa mkoa wa Rift Valley. Akataja maeneo ya Molo kuwa sehemu zilizokuwa zimeathiriwa na nyumba za watu zilikuwa zimeteketezwa. Kama hawa maaskofu wa sasa, serikali ya Daniel Arap Moi pia ilimkosoa Ndingi na kusema kuwa matamshi yake yalilenga kuigawanya nchi. Mkuu wa Mkoa wa Rift Valley siku hizo akasema Ndingi alikuwa mdanganyifu.

Maaskofu hawa wametuonyesha kitu kimoja, kuwa dhamira yao si tu kujali masilahi ya waumini wao bali wanaangazia pia matakwa ya Kenya kwa jumla.